Friday, May 28, 2010
MRAMBA AMVAA MWAPACHU TANGA
Na Benedict Kaguo,Tanga.
VUGUVUGU la uchaguzi katika kuwania kiti cha Ubunge katika Jimbo la Tanga mjini limeingia katika sura mpya baada ya Kijana mwenye umri wa miaka 25,Benson Mramba kujitosa kuwania kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumkabili Mbunge wa sasa Bw Bakari Mwapachu.
Kijana huyo aliyehitimu Shahada ya Uhandisi katika fani ya teknolojia ya habari na mawasilino kutoka Chuo cha St Joseph College Of Engineering and Technology jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili,Mramba alisema ameamua kujitosa katika kinyanganyiro hicho cha ubunge ili kuleta mabadiliko katika jimbo ambalo limekuwa likishikiliwa na wazee kwa muda mrefu.
Alisema licha ya kuthamini mchango wa wazee bado kuna kila sababu ya vijana kupata nafasi ili kuwasilisha mawazo mapya na mbadala katika kuharakisha maendeleo ya jimbo la Tanga ikizingatiwa kuwa hivi sasa ni karne ya 21 inayokwenda kasi na utandawazi na ukuaji wa kasi ya sayansi na teknolojia.
Alisema Tanga ni Manispaa ya kwanza katika nchi ya Tanzania hivyo ni lazima kupata viongozi wapya watakaoweza kurejesha hadhi iliyopotea kwa miaka mingi hasa na kuporomoka kwa uchumi hasa kufa viwanda,bandari,reli na michezo mbalimbali.
Alisema kwa sasa wananchi wa Tanga wanahitaji wawakilishi wataoweza kusimamia kimamilifu fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo TASAF,pamoja na usimamizi makini ya barabara zilizopo jijini Tanga ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi kila siku.
Alisema ikiwa atachaguliwa kuwa Mbunge atahakikisha anakuwa karibu na wananchi katika kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wake ikiwemo miradi ya Serikali Kuu na Halmashauri akitolea mfano EPZA na kuwahimiza wananchi wa Tanga kuwaunga mkono wagombea wa chama hicho ili kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya Jiji la Tanga.
No comments:
Post a Comment