Na Ismail Ngayonga
Maelezo
Dar es Salaam
WATANZANIA na wadau wa maendeleo nchini wamehimizwa kujitokeza na kuwekeza katika vivutio vilivyopo badala ya fursa hizo kuwaachia wageni kutoka nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano wa uwekezaji katika ukanda wa ziwa Tanganyika unaotajiwa kufanyika tarehe 17 oktoba mwaka huu.
Mhandisi Manyanya alisema wakati umefika kwa Watanzania kujitokeza na kuwa vinara katika sekta ya uwekezaji na kamwe wasitishwe na suala la uwezo, kwani katika mipango iliyopo inawasaidia pia wenye uwezo mdogo wa kuwekeza.
“Mikoa iliyopo katika ukanda wa ziwa Tanganyika ambayo ni Kigoma, Rukwa na Katavi ina fursa nyingi za uwekezaji, hivyo kila Mtanzania anahimizwa kuwekeza hata kama ana uwezo mdogo kifedha yapo baadhi ya maeneo unayoweza kuwekeza” Alisema Mhandisi Manyanya.
Alisema mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ni miongoni mwa mikoa yenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa ukanda huo wadau wote wa ndani na nje ya nchi wana fursa sawa ya uwekezaji kupitia mipango iliyopo.
Manyanya alisema kwa muda mrefu ukanda wa ziwa Tanganyika tangu enzi ya ukoloni umesifika kwa miundombinu duni ya huduma za kiuchumi na kijamii, hatua hiyo iliyosababisha mikoa yake kusahaulika katika harakati za maendeleo ya mawasiliano ya barabara, usafiri wa majini, reli, usafiri wa ndege pamoja na mawasiliano ya simu, runinga na redio.
Aliongeza kwa kutambua changamoto hizo, Serikali ya awamu ya nne imefanya kazi kubwa katika kufungua ukanda huo kwa kujenga miundombinu ya barabara za lami, viwanja vya ndege, bandari katika ziwa Tanganyika, upatikanaji wa umeme wa uhakika, pamoja na kuboresha huduma za jamii.
Kwa mujibu wa wa Mhandisi Manyanya alisema kutokana na mabadiliko hayo yaliyofanyika katika ukanda huo, ni fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuingia katika mikoa hiyo ili kuwekeza na hatimaye kuharakisha maendeleo ya wananchi.
“Wawekezaji wenye uzoefu wa biashara za hoteli za kitalii wanakaribishwa kujenga hoteli katika miji ya Kigoma, Mpanda, Sumbawanga, Mwambao mwa ziwa Tanganyika; pamoja na ujenzi wa mahoteli katika mbugas za hifadhi ya katavi, mahale na Gombe” alisema Manyanya.
Waliosoma Kusini waaswa kuchangia elimu
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Lindi Mjini, Salum Baruany amewashauri watu waliowahi kusoma katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania kushirikiana katika kufanikisha tamasha la kuchangia maendeleo ya elimu kwa ajili ya mikoa hiyo.
Baruany aliyasema hayo juzi katika kikao cha maandalizi ya tamasha la kuchangia maendeleo ya elimu kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kilichofanyika Ukumbi wa Imasco, Temeke jijini Dar es Salaam.
Akiwa mmoja wa waalikwa wa vikao hivyo vya kila wiki, Baruany alielezea kukunwa kwake na ubunifu wa baadhi ya wanafunzi walioamua kuwahamasisha wenzao kukumbuka walikotoka kielimu, kwa lengo la kuwainua wengine.
“Nawapongeza sana. Ni wachache wanaoweza kukumbuka walikotoka, hasa kielimu. Hapa mmelenga, mikoa ya kusini iko nyuma kielimu, naamini wa kusaidia kupandisha hadhi ni ninyi wenyewe mliosoma kule na wadau wengine wanaoguswa na suala hili.
“Msikate tamaa, mtafanikiwa. Cha msingi ni kuwashirikisha na kuwashawishi wengine waliosoma ana kuwa karibu na mazingira ya kielimu ya mikoa hii. Nchi hujengwa na wananchi wenye moyo, nanyi kwa kuguswa kwenu, naamini elimu ya kusini itainuka kwa sababu ni vigumu mtu mmoja mmoja kuchangia na bado maendeleo ya kweli yakaonekana, bali kupitia mshikamano kama wenu,” alisema mbunge huyo.
Naye Mratibu wa tamasha hilo, Asanterabbi Mtaki, licha ya kumshukuru mbunge huyo kwa nasaha zake, aliwataka wadau wa elimu nchini kuungana na waliosoma mikoa ya kusini ili kufanikisha azma ya kuiinua kusini kielimu.
“Tangu awali tumeelezea hali ya elimu ya mikoa ya Kusini, kwa kweli si nzuri na inahitajika nguvu ya ziada, ndiyo maana tumeungana kuhakikisha tunafanikisha kitu kwa ajili ya shule za kusini na wanafunzi wake, hasa yatima, walemavu na wasiojiweza ili wapate haki ya kupata elimu bora,” alisema Mtaki.
Alisisitiza kuwa, kasi ya maandalizi ya tamasha hilo inaridhisha na kuongeza kuwa, nafasi ya waliosoma kusini kuchangia mawazo bado ipo, hasa kupitia vikao vya kila mwisho wa wiki vinavyofanyika ukumbi wa Imasco.
No comments:
Post a Comment