Wednesday, March 14, 2012

WABUNGE KUCHAGUA WAWAKILISHI WA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI KATIKA MKUTANO WA SABA WA BUNGE

Katibu wa Bunge anatoa Taarifa kwa Umma kwamba, Uchaguzi wa wajumbe tisa (9) watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia tarehe 10 hadi 20 Aprili, 2012.
Uchaguzi huo wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki unafanyika kwa kuzingatia kuwa maisha ya Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006, yatafikia ukomo wake 04 Juni, 2012.
Pamoja na Taarifa hii, Katibu wa Bunge ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo, atatoa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusika, kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni tarehe 10 Aprili, 2012, saa kumi (10.00) Jioni, na pia kuhusu siku ya uchaguzi ambayo ni tarehe 17 Aprili, 2012 saa tano (5.00) Asubuhi, mara au mapema baada ya Kipindi cha Maswali.
Aidha, katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge pia atatoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na Wagombea wa Vyama vyote vya Siasa vyenye uwakilishi Bungeni kuhusiana na Uchaguzi huo, kwa ajili ya kuviwezesha kuanza mchakato wa kuwapata Wagombea kupitia Vyama hivyo, ambao majina yao yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.
Kwa Taarifa hii, watu ambao wanazo sifa za kugombea na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wanaweza kuanza mchakato wa kuteuliwa kuwa wagombea wa uchaguzi huo, kupitia Vyama vyao vya Siasa.
Taarifa hii imetolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge

No comments:

Post a Comment