Wednesday, March 14, 2012

Meneja mkuu wa Shirika la meli la Zanzibar tawi la Dar es salaam aomba meli mpya

Nafisa Madai Dar es salaam

Meneja mkuu wa Shirika la meli la Zanzibar tawi la Dar es salaam Mauwa Mohammed Abrahman ameiomba Serikali ya Zanzibar iwapatie meli mpya za abiria na meli za mizigo ili waweze kwenda sambamba na ushindani wa kibiashara na kupanua soko la Shirika hilo ambalo litaongeza kipato na kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato.

Akitoa taarifa za Shirika lake mbele ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi iliyofika jijini Dar res salaam kwa lengo la kukagua shughuli zinazoendeshwa na shirika hilo, amesema kuwa kwa sasa Shirika linajiendesha kwa hasara kutokana na kukosa uwakala wa meli nyingi zilizopo nchini na meli za kigeni na hivyo kulikosesha mapato Shirika ambayo yangeweza kupunguza changamoto zilizopo.

Aidha meneja huyo amesema hivi sasa Shirika lake limo katika mchakato wa kutafuta mbinu ya kuliendeleza kwa kutafuta vitega uchumi vitakavyo liwezesha shirika hilo kuongeza mapato yake ikiwemo kuboresha majengo ya Shirika hilo na hatimae kuyakodisha kwa wadau mbali mbali.

Akizungumzia suala la uwakala Meneja huyo amesema tawi limo mbioni kufuatilia leseni ya uwakala na kwa sasa tayari limekuwa likifuatilia kwenye makampuni ya meli ili kupata uwakala na pindi wakifanikiwa kupata leseni watapatiwa kazi hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Makame Mshimba Mbarouk amesema ipo haja kwa Serikali kuharakisha kununua meli zitakazilisaidia Shirika hilo liweze kurudisha hadhi yake ya awali.

Aidha alisema Serikali kuu iingilie kati katika kulitafutia Shirika jengo la uhakika kutokana na changamoto zilizopo hivi sasa za kukodi majengo ya ofisi ambapo majengo hayo hulipiwa kodi kubwa. Pia, ukosefu huo wa majengo ya kudmu unasababisha usumbufu mkubwa kwa watendaji wa Shirika kutokana na kuhamishwa hamishwa katika majengo wanayoyatumia.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Issa Haji Ussi (Gavu) ameiambia Kamati hiyo kuwa Shirika hivi sasa limekuwa likiyumba kimapato kwa vile vyombo vilivyopo ni vichache na chakavu kiasi ambacho vinashindwa kumudu ushindani wa kibiashara.

Hata hivyo amesema azma yaSserikali ya kununua meli mpya ipo pale pale na tayari hatua za mwisho zimeshakamilika za utafutaji wa meli hiyo ili iweze kutoa hudUma kwa wananchi.

Kamati hiyo pia ilipata fursa ya kuzungumza na wakuu wa Chuo cha Mabaharia (DMI) na kukitaka chuo hicho kutoa mashirikiano makubwa kwa Mamlaka ya usafiri wa Baharini (ZMA) kwa kuwasaidia katika utunzi wa Kanuni za Mamlaka hoyo zitakazosaidia kuongoza uendeshaji wa biashara za meli na mambo yake yote.

Ziara hiyo ya siku mbili imekuwa na mafanikio makubwa kwa wajumbe wa kamati hiyo kujifunza masuala mbali mbali pamoja na kutoa ushauri katika sehemu walizotembelea

No comments:

Post a Comment