Wednesday, March 14, 2012

WACHEZAJI 5 WAFYEKWA YANGA

KAMATI YA LIGI YAADHIBU WACHEZAJI 5 YANGA
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Dar es Salaam jana (Machi 12 mwaka huu) imetoa adhabu kwa klabu mbalimbali na wachezaji sita wakiwemo watano wa Yanga.
Villa Squad imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi namba 122 dhidi ya Azam iliyochezwa Februari 15 mwaka huu Uwanja wa Chamazi.
Pia klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi namba 129 dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Februari 19 mwaka huu Uwanja wa Manungu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 8(13) ya ligi hiyo.
Nayo Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi namba 132 dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu. Pia klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(d) baada ya kuoneshwa kadi kuanzia tano kwenye mechi hiyo.
Mchezaji Juma Mohamed wa Polisi Dodoma amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kuwashambulia watazamaji kwa chupa ya maji katika mchezo namba 114 kati ya timu yake na Villa Squad uliochezwa Februari 11 mwaka huu.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga amefungiwa mechi sita za Ligi Kuu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumshambulia mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi hiyo namba 132.
Wachezaji wengine wa Yanga walioadhibiwa kutokana na mechi hiyo ni Nurdin Bakari amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000, Omega Seme amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000, Jerryson Tegete amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000.
Stephano Mwasika amefungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja kwa kumpiga mwamuzi Nkongo. Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu.
Kamati ya Ligi imempongeza nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na mshambuliaji wa timu hiyo Hamis Kiiza kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi. Pia imempongeza kocha Kostadin Papic wa Yanga kwa kukemea vurugu zilizofanywa na wachezaji wake.
Pia Kamati ya Ligi imeiagiza Sekretarieti kutoa waraka kwa makamishna wote wa ligi juu ya utaratibu wa wageni rasmi wakati wa mechi za ligi.
Powered by Sorecson : Creation de site internet
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF

No comments:

Post a Comment