Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imeitaka
Serikali kuwawajibisha mara moja mawaziri, manaibu waziri na watendaji
wakuu wa Serikali na mashirika ya umma ambao wametajwa kuhusika na
matumizi mabaya ya fedha za umma ama kushindwa kusimamia rasilimali za
taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Anna Kikwa (PICHANI) katika
taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari. Aidha amemtaka mkuu
wa nchi awafute kazi watendaji wanaotumia vibaya fedha za umma na
kuwaongezea wananchi umasikini, ili iwe fundisho kwa watendaji wa
Serikali wenye tabia kama hiyo na wachukuliwe hatua za kisheria.
Hata hivyo TGNP imeishauri Serikali
kuboresha mifumo ya kusimamia rasilimali za nchi yetu ili wananchi wote
waweze kufaidi keki ya taifa kwa sababu mara zote Serikali imekuwa
ikisema Tanzania hatuna rasilimali lakini hali halisi ni kwamba
rasilimali za taifa zinaliwa na mafisadi wachache wa ndani na nje ya
nchi.
Katika hatua nyingine, mtandao huo umetoa
pongezi kwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika
ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Hesabu za
Serikali Kuu, Ardhi Maliasili na Utalii kwa kusimamia vema na kudhibiti
matumizi mabaya ya fedha za serikali zinazotokana na walipa kodi na
kuwasilisha ripoti zao Bungeni ambazo zimeibua uozo mkubwa na kujenga
mjadala mpana unaotaka uwajibikaji kwa wanaohusika.
“Tunawapongeza pia baadhi ya wabunge
walioshiriki katika mijadala kwa kuzijadili ripoti hizo kwa undani
bila kujali urafiki, itikadi za kisiasa, hasa ile ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuibua uozo uliojificha na
kusimamia maslahi ya Taifa.” amesema Bi. Kikwa katika taarifa hiyo.
“Tumeshuhudia mara kadhaa kupitia vyombo
vya habari wabunge wakiacha itikadi zao za kisiasa na kusimamia kwa
dhati dhana ya kushinikiza uwajibikaji katika vyombo vinavyohusika
kutokana na ufisadi kama Richmond, Dowans nk. Hata hivyo, TGNP kwa muda
mrefu tumekuwa tukipinga ubadhirifu wa fedha za umma na kudai haki ili
kutokomeza ufisadi uliokithiri, lakini bado ufisadi umezidi kushamiri
hasa katika Wizara na taasisi za umma.
“Sisi kama wanaharakati tunasema kuendelea
kwa ufisadi ni aibu kwa serikali iliyoko madarakani, TGNP tuko mstari
wa mbele kushinikiza rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wote,
hasa walioko pembezoni, kamwe hatutanyamazia aina yoyote ya ubadhirifu
na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya wananchi zilizotengwa kwa ajili
ya maendeleo ya wananchi.” Imesema taarifa hiyo.
"Tumeshuhudia wanawake na wasichana
wakiendelea kuwa maskini na kukumbana na mifumo kandamizi kwa kukosa
haki za kufikia huduma za msingi kama vile maji, barabara, afya, elimu,
kilimo, utawala bora n.k. Fedha zinazopotea zinatokana na kodi za
wananchi na jamii ina haki ya kuhoji uwajibikaji na wahusika wanatakiwa
kuchukuliwa hatua za kisheria," imeongeza taarifa hiyo kwa vyombo vya
habari.
Vilevile tunawapongeza wabunge wote
walioshiriki kwa dhati katika zoezi la kusaini kusudio la kutaka
viongozi waliotajwa/kutuhumiwa kwenye ripoti hizo kuwajibika. Ili
kuonesha dhana ya uwajibikaji na utawala bora unaozingatia misingi ya
haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment