Mhariri Mkuu wa Mtandao wa Thehabari.com, Joachim Mushi akifanya
mahojiano na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Watoto Ummy Mwalimu jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Watoto, Ummy Mwalimu
(kulia) akimadilishana kadi za mawasiliano na Mhariri Mkuu wa
Thehabari.com, Joachim Mushi mara baada ya mahojiano ofisini kwake leo
jijini Dar es Salaam.
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu jana
amejitolea kumsaidia mtoto ambaye mzazi wake alishindwa kumpeleka shule
baada ya kufaulu kwa kile kukosa ada ya shule.
Akizungumza na Mhariri Mkuu wa Mtandao wa Thehabari.com, Joachim
Mushi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam amesema ameguswa na habari
hiyo iliyotolewa na mtandao huu juzi, hivyo yupo tayari kumsaidia mtoto
huyo nawengine watakao kuwa na matatizo kama hayo eneo hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri Mwalimu, ambaye pia ni Mbunge wa Viti
Maalumu kutokea Mkoa wa Tanga amesema anaamini mama wa mtoto huyo
alikuwa muoga kuwasiliana na viongozi wa wilaya hiyo ya Handeni kwani
wangelimsaidia na mtoto huyo kujiunga na shule.
"Kwanza napenda kuwapongeza kwa kuibua changamoto kama hizi,
kimsingi nimeguswa na habari hiyo ya mtoto kushindwa kujiunga na shule
kwasababu mzazi wake hana uwezo...naomba mnipe mawasiliano ili tuangalie
namna ya kumsaidia," alisema Naibu Waziri huyo.
Alisema ipo haja ya halmashauri kufuata ushauri wa Serikali kwa kile
kutenga asilimia 5 ya mapato yao kuwawezesha wanawake kupitia mfuko wa
maendeleo ya wanawake, kwani endapo akinamama watawezesha wanaweza
kufanya mabadiliko hata katika changamoto kama hizo.
"Unajua ukimuwezesha mwanamke unakuwa umeiwezesha jamii...endapo
kila wilaya ikikubali kutenga asilimia 10 ya mapato yake, kwa ajili ya
mfuko wa maendeleo ya wanawake na ule wa vijana kwa kugawa asilimia
tano tano kila upande tutasaidia mambo mengi, zikiwemo changamoto za
maisha katika familia," alisema Mwalimu.
Juzi mtandao wa Thehabari.com pamoja na mitandao mingine washirika
wa Thehabari.com walichapisha habari ya mmoja wa wanafunzi
waliochanguliwa kujiunga na masomo mwaka huu kushindwa kuendelea na
shule baada ya mzazi wake mmoja (mama) kushindwa kumgharamia.
Mtandao wa Thehabari.com unafanya mawasiliano na mzazi wa mtoto huyo
na kuangalia namna ya kuwakutanisha na baadhi ya wasamaria waliojitolea
kubeba mzigo wa masomo kwa kijana huyo. Mtandao huu utaendelea
kuwajulisha taarifa zaidi za tukio hili hadi pale mtoto atakapo jiunga
na shule.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (wwww.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment