Tuesday, June 26, 2012

MASHALI SASA AWATAKA CHEKA, KASEBA



Mashali akivalishwa mkanda wake wa ubingwa baada ya kuutetea jana kwa kumtwanga TKO raundi ya tano Maisha


Na Prince Akbar
BAADA ya kumtwanga kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tano Samson Maisha wa Mbeya, bingwa wa Taifa wa TPBO, Thomas Mashali 'Simba wa Teranga' amesema anamtaka mshindi wa pambano kati ya Japhet Kaseba na Francis Cheka apande naye ulingoni, ili adhihirishe yeye ndiye ‘king’ wa ndondi Tanzania.
Mashali akiwa amemdondosha Maisha jana
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese jana baada ya ushindi wake huo, Mashali alisema kwamba anaamini kwa sasa katika nchi hii hana mpinzani na ameomba yeyote atakayeshinda kati ya Kaseba na Cheka asikwepe kupanda naye ulingoni.
“Huyu mtoto (Maisha), si saizi yangu, wamempakazia tu, baada ya kuona mabondia wote wa Dar es Salaam sasa hivi wananiogopa, nilikuwa nampiga huku namhurumia, na bado amefia katikati ya safari (raundi ya tano). Namtaka mshindi kati ya Kaseba na Cheka,”alisema Mashali.  
Katika pambano hilo la jana la uzito wa Middle, Mashali alimzidi uwezo mpinzani wake kuanzia raundi ya kwanza na katika raundi ya tano alimkalisha chini kwa ngumi kali ya mkono wa kulia.
Maisha alijitutumua kuinuka ili aendelee na pambano, lakini alionekana dhahiri hajiwezi na ndipo Kocha wake, Bagaza Mambane akarusha taulo ulingoni. Hata hivyo, Maisha anaonekana ni bondia mzuri akipata mazoezi zaidi na ujanja wa katika masumbwi. 

No comments:

Post a Comment