Wednesday, June 6, 2012

MBUNGE WA SEGEREA AWATAKA WADAU WA ELIMU KUJITOKEZA KATIKA HARAMBEE YA KATA YA KIPAWA KATIKA HOTELI YA HYATT KILIMANJARO


Diwani wa Kata ya Kipawa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam, Bonah Kaluwa (kushoto), akiwa katika moja ya mikutano ya maendeleo kwenye kata yake. Kulia ni Katibu  wa Kata hiyo Amina Sabo na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Karakata, Greyson Malick. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)
 
 
Na Dotto Mwaibale

MBUNGE wa Jimbo la Segerea Dk. Makongoro Mahanga amewataka wadau wa elimu kujitokeza leo kuchangia mfuko wa elimu wa Kata ya Kipawa katika harambee itayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempiski.

Alisema Kata ya Kipawa ni moja ya kata iliyopo katika jimbo la Segerea na Manispaa ya Ilala zenye upungufu mkubwa wa miundombinu na vifaa katika shule zake za msingi na za sekondari za serikali.

Alisema upungufu huo ni pamoja na uchache wa shule, upungufu wa madarasa, madawati, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, meza na viti vya walimu, maabara na nyumba za walimu.
" Upungufu huu wa mahitaji katika shule za kata ya Kipawa, ni tatizo la mkoa mzima wa Dar es Salaam, na wilaya nzima ya Ilala hivyo ni wajibu wetu kusaidia". alisema Mahanga

Alisema katika suala la elimu serikali ya awamu ya nne imefanya mengi mazuri ingawa bado kuna changamoto kadhaa ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam,  kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaosoma shule za awali, shule za msingi na shule za sekondari.

Aliongeza kuwa kwa sasa kuna wanafunzi 26,121 wa shule za awali katika mkoa wa Dar es Salaam, kati yao wanafunzi 7,499 wako katika wilaya ya Ilala. Mkoa wa Dar es Salaam pia kwa sasa una wanafunzi 510,269 wanaosoma shule za msingi, kati yao wanafunzi 152,135 ni wa wilaya ya Ilala.

Alisema  kuna wanafunzi 204,684 wa shule za sekondari katika mkoa wa Dar es Salaam, kati yao wanafunzi 57,890 wako katika wilaya ya Ilala. Katika mkoa wa Dar es Salaam, kuna shule 315 za sekondari, kati yake shule 135 ni za serikali.

" Nguvu za wananchi zimetumika sana hasa katika ujenzi wa shule za sekondari nchini na kuungwa na serikali ambapo kwa mkoa   wa Dar es Salaam kati ya shule hizo za serikali 135, shule 124 ni za wananchi zilizojengwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri za wilaya." alisema Mahanga.

Alisema shule hizo 124 za wananchi za mkoa wa Dar es Salaam, wilaya ya Ilala ina shule 40 za sekondari za wananchi, ambazo karibu zote zimejengwa kuanzia mwaka 2006.

Alisema Shule hizo nyingi zinachangamoto na upungufu wa vyumba vya madarasa 5,526, kati yake wilaya ya Ilala ina upungufu wa madarasa 1,459, ofisi za walimu 466,nyumba za walimu 14,788.

Alisema katika mkoa wa Dar es Salaam kuna upungufu wa madawati 58,764 kwa shule za msingi na 45,349 kwa shule za sekondari. Kati ya hizo wilaya  ya Ilala ina upungufu wa madawati 18,030 kwa shule za msingi na madawati 19,534 kwa shule za sekondari.
Alisema matundu ya vyoo 18,558 yanahitajika kwa mkoa wa Dar es Salaam, huku wilaya yenu hii ya Ilala ikihitaji matundu ya vyoo 4,886.

Alisema katika uchangia wa elimu hatuwezi kuiachia serikali pekee, kwani uwezo wa serikali yetu ni ndogo hivyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa kata ya Kipawa wakiongozwa na diwani wao, Bonnah Kaluwa kwa kubuni mradi wa uchangiaji miundombinu ya shule katika kata hiyo.

No comments:

Post a Comment