Diwani wa Kata ya Kipawa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam, Bonah Kaluwa
(kushoto), akiwa katika moja ya mikutano ya maendeleo kwenye kata yake.
Kulia ni Katibu wa Kata hiyo Amina Sabo na Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa wa Karakata, Greyson Malick. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)
Na Dotto Mwaibale
MBUNGE wa Jimbo la Segerea Dk. Makongoro Mahanga amewataka wadau wa
elimu kujitokeza leo kuchangia mfuko wa elimu wa Kata ya Kipawa katika
harambee itayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika
Hoteli ya Kilimanjaro Kempiski.
Alisema Kata ya Kipawa ni moja ya kata iliyopo katika jimbo la
Segerea na Manispaa ya Ilala zenye upungufu mkubwa wa miundombinu na
vifaa katika shule zake za msingi na za sekondari za serikali.
Alisema upungufu huo ni pamoja na uchache wa shule, upungufu wa
madarasa, madawati, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, meza na viti vya
walimu, maabara na nyumba za walimu.
" Upungufu huu wa mahitaji katika shule za kata ya Kipawa, ni
tatizo la mkoa mzima wa Dar es Salaam, na wilaya nzima ya Ilala hivyo ni
wajibu wetu kusaidia". alisema Mahanga
Alisema katika suala la elimu serikali ya awamu ya nne imefanya
mengi mazuri ingawa bado kuna changamoto kadhaa ambapo kwa mkoa wa Dar
es Salaam, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaosoma shule za
awali, shule za msingi na shule za sekondari.
Aliongeza kuwa kwa sasa kuna wanafunzi 26,121 wa shule za awali
katika mkoa wa Dar es Salaam, kati yao wanafunzi 7,499 wako katika
wilaya ya Ilala. Mkoa wa Dar es Salaam pia kwa sasa una wanafunzi
510,269 wanaosoma shule za msingi, kati yao wanafunzi 152,135 ni wa
wilaya ya Ilala.
Alisema kuna wanafunzi 204,684 wa shule za sekondari katika mkoa
wa Dar es Salaam, kati yao wanafunzi 57,890 wako katika wilaya ya Ilala.
Katika mkoa wa Dar es Salaam, kuna shule 315 za sekondari, kati yake
shule 135 ni za serikali.
" Nguvu za wananchi zimetumika sana hasa katika ujenzi wa shule za
sekondari nchini na kuungwa na serikali ambapo kwa mkoa wa Dar es
Salaam kati ya shule hizo za serikali 135, shule 124 ni za wananchi
zilizojengwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri za
wilaya." alisema Mahanga.
Alisema shule hizo 124 za wananchi za mkoa wa Dar es Salaam, wilaya
ya Ilala ina shule 40 za sekondari za wananchi, ambazo karibu zote
zimejengwa kuanzia mwaka 2006.
Alisema Shule hizo nyingi zinachangamoto na upungufu wa vyumba
vya madarasa 5,526, kati yake wilaya ya Ilala ina upungufu wa madarasa
1,459, ofisi za walimu 466,nyumba za walimu 14,788.
Alisema katika mkoa wa Dar es Salaam kuna upungufu wa madawati
58,764 kwa shule za msingi na 45,349 kwa shule za sekondari. Kati ya
hizo wilaya ya Ilala ina upungufu wa madawati 18,030 kwa shule za
msingi na madawati 19,534 kwa shule za sekondari.
Alisema matundu ya vyoo 18,558 yanahitajika kwa mkoa wa Dar es
Salaam, huku wilaya yenu hii ya Ilala ikihitaji matundu ya vyoo 4,886.
Alisema katika uchangia wa elimu hatuwezi kuiachia serikali
pekee, kwani uwezo wa serikali yetu ni ndogo hivyo alitumia fursa hiyo
kuwapongeza viongozi wa kata ya Kipawa wakiongozwa na diwani wao, Bonnah
Kaluwa kwa kubuni mradi wa uchangiaji miundombinu ya shule katika kata
hiyo.
No comments:
Post a Comment