Monday, July 30, 2012

GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.

Katika matoleo yake hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Mhariri, mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.


Uamuzi wa Serikali

Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai, 2012.


Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na wajibu.


Kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.

Imetolewa na

OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012

No comments:

Post a Comment