Monday, July 23, 2012

RC MANYANYA AMUOMBA WAZIRI WA MAJI PROF. JUMANNE MAGHEMBE KUUPA KIPAUMBELE MAALUM MKOA WA RUKWA KATIKA MIRADI YA MAJI



Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya waziri wa maji Prof. Jumanne Maghembe mkoani humo. kushoto ni katibu tawala wa mkoa Alhaj Salum Chima

NA RAMADHANI JUMA,
AFISA HABARI-SUMBAWANGA
MKUU wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya ameiomba serikali kuupatia kipaumbele maalum mkoa huo katika miradi ya maji kutokana na kukabiliwa na upungufu wa muda mrefu wa huduma hiyo.
Alitoa ombi hilo kwa waziri wa Maji Mh. Profesa Jumanne Maghembe wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya waziri huyo mkoa humo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa, licha ya tatizo hilo kuwa kubwa na la muda mrefu, huenda upungufu huo wa huduma ya maji safi ukaongezeka mara dufu mara baada ya ujenzi wa barabara zinazounganisha mkoa huo na ule wa Mbeya na Katavi kukamilika kwa kiwango cha lami, hali itakayosababisha idadi ya watu kuongezeka kutoakana na shughuli za kiuchumi kushamiri.
Manyanya alipendekeza serikali kutekeleza miradi midogomidogo ya maji ya visima mkoani humo ili kuwaharakishia wakazi wake huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake, waziri Profesa Maghembe iliahidi kuwa, serikali itatekeleza miradi ya maji katika vijiji 10 vya kila wilaya ya Mkoa huo ambazo ni Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
Alisema kuwa, utekelezaji wa mpango huo utaanza na vijiji vitatu katika kila wilaya na tayari shilingi bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili awamu ya kwanza kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji ya Laela, Matai na kijiji cha Nankanga.

No comments:

Post a Comment