Monday, August 13, 2012

AUAWA KISHA KUFUKIWA KATIKA SHIMO NYUMA YA CHOO


RPC Dodoma, SACP Zelothe Stephen
Na Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.

Mwanafunzi wa Darasa la Saba shule ya msingi Hogolo, aliyefahamika kwa jina la Matha Mazoea Mwenye umri wa Miaka (14)  ameuawa kwa kunyongwa na kufukiwa kwenye shimo nyuma ya nyumba yao karibu na choo baada ya kubakwa.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Zelothe Sephen alisema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 11/08/2012 majira ya saa 08:00 asubuhi katika mtaa wa Ikulu Kijiji cha Hogolo Kata ya Hogolo tarafa ya Zoisa Wilaya ya Kongwa.

 “Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kwani marehemu alikuwa amevunja uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu aliyejulikana kwa jina la Heri Aboubakar na kuanzisha uhusiano na mpenzi wake mpya aliyefahamika kwa jina la Wilfredy Muhaha @ Kabo mwenye miaka (17) “ Alielezea Kamanda Zelothe

Katika tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji hayo ambao ni Asha Jafari Mohamed mwenye umri wa miaka 16, mkulima, mkazi wa Mtaa wa Nyerere Hogolo ambaye ni rafiki wa marehemu na Rino Mazoea mwenye umri wa miaka 21, Mkulima, Mkazi wa Ikulu Hogolo Wilayani Kongwa ambaye ni kaka wa marehemu.

Bw. Zelothe alieleza kwamba  ili kufanikisha uchunguzi wa awali Jeshi la Polisi pia Wilayani humo linamshikilia  mpenzi mpya wa marehemu Bw. Wilfredy s/o Muhaha  pamoja na kumtafuta mpenzi wa zamani wa  marehemu  Bw. Heri s/o Aboubakar ambaye amekimbia kijijini hapo na hajulikani alipo mpaka sasa.

Aidha kamanda Zelothe alisema Katika tukio hilo Kaka wa marehemu ambaye  anashikiliwa na Jeshi la Polisi, katika maelezo yake ya awali alidai kusikia  purukushani zikitokea usiku wa tukio hilo la mauaji lakini hakuweza kutoka usiku huo ili kushuhudia nini kinaendelea.

Kamanda Zelothe alisema Marehemu alikuwa akiishi na babu na bibi yake hapo Kijijini na kwamba siku ya tukio walikuwa wameondoka kwenda katika Vijiji vya jirani, ambapo bibi yake na marehemu alikuwa amekwenda  Kongwa kwa ajili ya kujengea makaburi na babu yake alikwenda kijiji cha  Banyi banyi kwa Shughuli za kutemebelea wagonjwa.

Wakati huo huo Gari lenye namba za usajili T. 750 AEU aina ya TOYOTA CHASER likiendeshwa na Kenedy James mwenye umri wa miaka 48, Mkazi wa Mpwapwa liliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha Salum Kaduma mwenye umri wa miaka (13) Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Katika shule ye sekondari ya Mpwapwa, na kusababisha kifo chake.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma alisema ajali hiyo ilitokea mnamo tarehe 12/08/2012 majira ya saa 09:00 asubuhi katika eneo la Kisima Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa magurudumu mawili ya upande wa kulia kitu kilichopelekea gari hilo kuacha njia na kupinduka.” Aliongeza Bw. Zelothe.

No comments:

Post a Comment