Tuesday, August 28, 2012

DIDIER DROGBA, NICOLAS ANELKA WAGEUKA MIZIGO CHINA

Drogba kushoto, akifanya mazoezi na mshambuliaji mwenzake wa Shanghai Shenhua, Nicolas Anelka

 Didier Drgogba akiwajibika katika moja ya mechi za klabu ya Shanghai Shenhua
 Nicolas Anelka akiwa katikamoja ya mechi za klabu yake ya Shanghai Shenhua ya China


SHANGHAI, China

WASHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba na Nicolas Anelka wanaweza kuuzwa na Shanghai Shenhua ya China kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji zinazoikabili klabu hiyo na kuzua mgogoro miongoni mwa wanahisa.

Mwenyekiti wa Shanghai Shenhua, Zhu Jun, ambaye ana asilimia 28.5 ya hisa, ilikuwa alipe tu sehemu ya gharama za kila siku za klabu ambapo kwa madai yake udhibiti wa mahitaji na matumizi ya siku haukuweza kudhibitiwa, gazeti la China Daily limefichua.

Makubaliano ya awali yalikuwa, kama Zhu angewekeza dola milioni 23.6 katika klabu hiyo kwa zaidi ya miaka miwili, hisa zake zitapaswa kupanda na kufikia zaidi ya asilimia 70, gazeti hilo lilifichua.

Gazeti jingine la Oriental Sports Daily liliripoti kuwa Zhu aliwekeza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 94 katika kipindi cha miaka mitano na nusu, wakati makampuni yanayomilikwa na serikali hayakutumia chochote.

"Hali imekuwa tatanishi na jambo baya zaidi kwetu ni majukumu mazito miongioni mwetu," taarifa rasmi ya klabu ilisema na kuongeza: "Tatizo kubwa ni kwamba, uendeshaji wa masuala ya kipesa na kazi kwa klabu hayawezi kufanywa nje ya taratibu.

"Jambo hilo limezua sintofahamu na kuweka shakani mustakabali wa maendeleo na ustawi wa Shenhua."

Kama hali ya mambo haitopatiwa ufumbuzi, Zhu, ambaye ndiye anayesaini cheki zote za malipo klabuni, anaweza kuamua kuweka kwenye soko la hisa, asilimia yake 28.5 ya hisa zake, kitu ambacho kitaathiri kwa kiasi kikubwa mapato na mishahara ya wachezaji.

Hali hiyo inazua shaka matarajio ya Drogba na Anelka kuweza kubakishwa Shenhua, kutokana na mishahara mikubwa ya pauni 300,000 kwa wiki wanazolipwa kila mmoja.

Pamoja na kutumia pesa nyingi kuisajili nyota wenye majina makubwa, Shenhua iko nafasi ya 10 kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya China, ikiwa na pointi 27 ilizovuna katika mechi 23, pointi 20 nyuma ya vinara Guangzhou Evergrande yenye pointi 47.

No comments:

Post a Comment