Wednesday, August 29, 2012

SERENGETI BOYS SASA KUIVAA MISRI



Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) sasa itaivaa Misri kwenye raundi ya pili ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 10 za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
 
Awali Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya kwanza dhidi ya Kenya, mechi ya kwanza ikichezwa Septemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) jana lilituma taarifa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) likielezea kujitoa kwenye michuano hiyo.
 
Serengeti Boys itaanzia nyumbani Oktoba 14 mwaka huu, wakati ya marudiano itachezwa nchini Misri kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu. Mshindi baada ya mechi hizo mbili ataingia raundi ya tatu ambayo ndiyo ya mwisho kabla ya kwenda Morocco.
 
Katika raundi ya tatu ambayo mechi zake zitachezwa katikati ya Novemba na ya marudiano mwisho mwa mwezi huo, mshindi kati ya Tanzania/Misri atacheza na mshindi wa mechi ya Congo Brazzaville dhidi ya Msumbiji/Zimbabwe ambazo zinapambana katika raundi ya kwanza.
 
Wachezaji wanaounda kikosi cha Serengeti Boys chini ya Kocha Jakob Michelsen ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu).
 
Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni).
 
Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu).
 
Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).

No comments:

Post a Comment