Saturday, August 18, 2012

MBWANA SAMATA, MPUTU KUIBEBA TP MAZEMBE KESHO?


Mshambuliaji Mtanzania Mbwana Samata wa TP Mazembe ya Congo-DRC (kulia) akiwajibika dimbani katika moja ya mechi za klabu hiyo.
 CAIRO, Misri

Katika mechi ya awali iliyopigwa Agosti 4 huko Stade TP Mazembe jijini Lubumbashi, Mazembe iliichapa Zamalek, shukrani kwa mabao ya Ngandu Kasongo dakika ya 70 na Mbwana Samata dakka ya 77

WASHAMBULIAJI Tresor Mputu na Mbwana Samata waliofunga mabao 10 kati ya 16 iliyofunga TP Mazembe hadi sasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho watakuwa katika jaribio la kuizamisha Zamalek nyumbani katika mechi ya nne hatua ya makundi.

Mputu na Samata, wamebeba matumaini ya Mazembe kuiduwaza Zamalek ya Misri ambao ni mabingwa wa zamani Afrika wanaonolewa na kocha Jorvan Vieira, pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Jeshi jijini Cairo.

Mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Slim Jedidi wa Tunisia, itatumiwa na Mafarao hao kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 2-0 mapema mwezi huu, huku ikipanga kutumia kisasi hicho kuitibulia Mazembe inayosaka pointi muhimu.

Kutokana na msimamo wa kundi B ulivyo, Zamalek haiwezi kubadili nafasi yake mkiani mwa kundi bila pointi, ingawa inaweza kuiharibia Mazembe iliyo na pointi nne kwenye nafasi ya pili, kama ilizonazo Berekum Chelsea inayoingia dimbani kuivaa Al Ahly kesho.

Al Ahly inaongoza kundi ikiwa na pointi tisa na kama itamudu kuichapa Berekum itajihakikishia nafasi ya kutinga nusu fainali, ambayo Mazembe inapigania ushindi wa angalau mechi mbili kati ya tatu za raundi ya pili kufuzu hatua hiyo.

Mapema juzi, Vieira Mbrazil anayeinoa Zamalek, alitangaza wakali 20 watakaobeba jukumu la kupigania heshima ya klabu hiyo dhidi ya Wakongo hao, ambapo alimtema kikosini winga Mohammed Abd Al Shafi na kumrudisha kiungo Ahmed aliyekwaruzana na kutemwa na kocha aliyepita Hassan Shehata.

Katika mechi ya awali iliyopigwa Agosti 4 huko Stade TP Mazembe jijini Lubumbashi, mabao mawili yaliyofungwa na Ngandu Kasongo dakika ya 70 na Mtanzania Samata dakka ya 77, yaliipa ushindi muhimu baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Berekum ya Ghana.

Kama itakubali kichapo katika mechi ya kesho, Zamalek itakuwa imepoteza rasmi nafasi ya kufuzu nusu fainali, ikiwa na mechi mbili mkononi, ambapo nyota wa Berekum Chelsea, Emmanuel Clottey anaongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu akiwa na mabao 12.

No comments:

Post a Comment