Friday, August 24, 2012

Rais Dk. Shein ahimiza wananchi wa Zanzibar kujitokeza kuhesabiwa, zoezi la Sensa keshokutwa



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akitoa taarifa maalum kwa wananchi kuhusu zoezi la kuhesabiwa la Sensa, litakalofanyika siku ya Jumapili, Agosti 26, mwaka huu, ambayo itawezesha na kufanikisha mipango ya
maendeleo kwa Taifa. (Picha ya Ramadhan Othman, Ikulu)


Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
 24.8.2012                                                                                          

RAIS  wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa matokeo ya sensa ndio yanayoipa Serikali taarifa halisi na ya kitaalamu juu ya idadi ya watu na taarifa nyengine muhimu katika kutayarisha mipango ya maendeleo.
 Dk. Shein aliyasema hayo leo katika taarifa yake aliyoitoa kupitia vyommbo vya habari kwa wananchi kuhusu umuhimu wa wananchi katika kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makaazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti, mwaka huu.

Kwa matiki hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa kujua idadi ya watu katika eneo fulani kunaiwezesha Serikali kukadiria mahitaji ya huduma kwa wakaazi wake ambapo kinyume chake ni kutoa huduma pungufu kwa vile hakuna takwimu sahihi ya wakaazi hao.

Dk. Shein alisema kuwa si jambo la kufurahisha kusikia kuwa baadhi ya watu ambao wanawashawishi watu wengie wasishiriki katika zoezi hilo muhimu na kusisitiza kuwa wananchi wa Zanzibar sio wageni katika zoezi hilo kwani wameshashiriki kwa vipindi kadhaa na kupata mafanikio ambapo sensa ya mwanzo iliyowajumuisha watu wote ilifanyika mwaka 1948.

Alisema kuwa suala la kuzingatia ni kuwa sensa haina uhusiano wo wote na matakwa ya watu kibinafsi bali ina lenga kuleta mafanikio kwa watu wote kwani hilo ni jambo la msingi sana kwa lengo la kuiwezesha  Zanzibar kujua idadi halisi ya wananachi wake na kuwafikishia maendeleo.

“Sote lazima tuweke mbele mapenzi na uzalendo kwa nchi yetu tukielewa kuwa sisi ndio wapangaji, watekelezaji na wasimamzi wa mipango yetu ya maendeleo kwani bila ya kushiriki katika utekelezaji wa majukumu hayo nchi yetu itawachwa nyuma na mataifa mengine yatasonga mbele kwa kasi, jambo ambalo siyo vyema kuliruhusu”, ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa mara nyengine tena kuwasihi wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu hapa nchini.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa sensa zote ni muhimu, lakini sensa ya mwaka huu ina umhimu wa kipekee kwa kuwa taarifa zitakazokusanywa zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na mwaka 2020 kwa Zanzibar pamoja na Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umasikini MKUKUTA na MKUZA.

Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, kisiasa, utawala bora, haki za binaadamu na ustawi wa jamii licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kadhaa.

Dk. Shein alisema kuwa taarifa kutoka Ofisi ya Rais inayoshughulikia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo zimebainisha mafanikio makubwa katika kukuza uchumi katika kipindi cha miaka miwili iyiliyopita.

Alieleza kuwa pato la jumla la mtu binafsi limeongezeka kutoka wastani wa Tsh. 782,000 mwaka 2010 hadi kufikia Tsh. 960,000 mwaka 2011. Aidha, taarifa za hivi karibuni zinaonesha kuwa uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa asilimia 6.8 katika mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 6.5 ya mwaka 2010.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa jitihada mbali mbali zimefanyika kupunguza tatizo la mfumko wa bei ambapo katika miezi ya mwanzo ya mwaka huu ilionekana hali  kuwa sio nzuri na kutokana na juhudi hizo mfumko wa bei umeweza kudhibitiwa hadi kufikia asilimia 9.4 kwa mwezi wa Juni kwani awali ya mwaka 2011 na 2012 ilifikia hadi asilimia 16.6.
Akiendelea kutaja mafanikio hayo, Dk. Shein alisema kuwa mafanikio yamejitokeza kwa upande wa ujenzi wa miundombinu, kuimarika kwa huduma za maji safi na salama na pia kuzidi kusambaa kwa huduma za umeme kwa wananchi wengi zaidi hasa wa vijijini.

Pia, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imepiga hatua katika uimarishaji wa sekta ya kilimo baada ya Serikali kutekeleza ahadi yake ya kutoa  ruzuku kwa wakulima ambapo asilimia 75 ya gharama imebebwa na Serikali.

Alieleza kuwa hatua iliyofikiwa hivi karibuni ya kuwandolea wananchi mchango wa Tsh. 40,000 kwa waja wazito wanaojifungua kwa njia ya operesheni, imetokana na kuwa na takwimu sahihi zenye kuonesha idadi yao na kiasi cha fedha kinachopatikana.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwashukuru viongozi wa ngazi mbali mbali katika jamii ambao muda wote wameendelea kuwahamasisha wananchi ili washiriki katika sensa ya mwaka huu, huku akiwashukuru wananchi wote kwa ushirikiano mkubwa walioutoa wakati wa maandalizi ya zoezi la sensa tangu lianze katika hatua mbali mbali.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa kwa azma ya kuitakia mema Zanzibar, ni vyema kila mtu ashiriki katika kuhesabiwa na kufanikisha zoezi hilo “Hii ni dhamana yetu sote”,alisema Dk. Shein.
Mbali na hayo Dk. Shein aliwataka Maafisa wa sensa na wote watakaoshiriki katika zoezi hilo kuwa na bidii ya kazi yao, nidhamu, ustahamilivu na uchangamfu wakati wote na wawafahamishe na wawaelimishe watu yanayopaswa kufanywa na maelezo yanayohitajika.

No comments:

Post a Comment