Monday, August 27, 2012

YANGA YAWASILI BILA MBUYU TWITE



 Baadhi ya wachezaji wa timu ya Yanga wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana wakitokea katika ziara ya michezo ya kirafiki nchini Rwanda


NaMwandishi Wetu

MASHABIKI wa soka nchini wameendelea kutoamini macho yao, baada ya Mabingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati Yanga leo kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere jijini Dar es Salaam ikitokea Kigali, Rwanda, bila ya beki wake mpya aliyecheza mechi za kirafiki nchini humo Mbuyu Twite.

Twite aliyesajiliwa na Yanga akiwa Rwanda na kisha kubaki huko hadi alipoungana na timu nchini humo na kucheza mechi hizo za kirafiki, alitarajiwa kutua jijini na Wanajangwani hao, ambapo mashabiki wa Yanga na wa Simba walisubiri ujio wake.

Kusubiriwa kwa hamu kwa Twite kunatokana na mkanganyiko aliozua katika usajili wake, ambapo awali alisajiliwa na kutambulishwa na Simba akitokea APR ya Rwanda alikokuwa akicheza kwa mkopo, kabla ya Yanga kutibua dili hilo na kumsainisha kupitia klabu yake ya zamani ya Lupopo ya DRC.

Licha ya kutowasilisha jina lake kwa TFF, Simba imeendelea kulia na Twite iliyemtangaza kuwa tapeli na kumfungulia jalada (RB) la wizi wa kuaminika wa dola za Kimarekani 30,000 za usajili, huku ikimtaka kurejesha fedha hizo mwenyewe kama alivyopewa.

Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo wakati msafara wa watu zaidi ya 40 Yanga, wakiwamo wachezaji 28 ulipopokelewa, Katibu Mkuu wa Yanga Mwesigwa Celestine, alisema kuwa, Twite atawasili nchini wakati wowote na kuwa amebaki Kigali akikamilisha baadhi ya mambo.

“Hakuna cha kumtish Twite kiasi cha kutoungana nasi kuja Dar, kuna taratibu muhimu anashugulikia. Atatua nchi wakati wowote na tutakuwa naye katika pambano letu na Coastal Union hapo Jumamosi,” alisema Mwesigwa akikana habari zilizozagaa uwanjani hapo kuwa alihofia kutiwa mikononi na Simba.

Katika mechi ya kwanza, Yanga iliyokuwa pia icheze na APR katika mechi hizo, iliichapa Rayon Sport mabao 2-1, shukrani kwa mabao ya washambuliaji Hamisi Kiiza na Simon Msuva, kabla ya juzi mabeki Stephano Mwasyika na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuipa ushindi dhidi ya Polisi.

Kocha Tom Saintfiet kwa upande wake alifurahishwa na ziara hiyo, akisema kuwa anaamini vipimo bora kuitoka kwa Rayon na Polisi, vimesaidia kuwaimarisha vijana wake, kuelekea Ligi Kuu ya Vodacom inayotarajiwa kuanza mwezi ujao.

“Licha ya kukosa fursa ya kuumana na APR, lakini najivunia changamoto ilizopata timu yangu kutoka kwa Rayon na Polisi. Ni timu bora na imara zilizotupa makali stahili na sasa tuko tayari kwa ligi,” alisema Saintfiet.

Msafara huo uliongozwa na Mwenyekiti, Yussuf Manji, Makamu wake, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ambao ni Mama Fatma Karume, Francis Mponjolwe Kifukwe na Seif Magari, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.

Mbelgiji Saintfiet, na Msaidizi wake Fred Felix Minziro, waliongoza benchi la ufundi lililojumuisha pia kocha wa makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh Saleh, Daktari, Sufiani Juma na mtunza vifaa Mahmoud Omary

No comments:

Post a Comment