Thursday, September 20, 2012

BALOZI WA KUDUMU WA TANZANIA UMOJA WA MATAIFA AWASILISHA HATI ZAKE KWA BAN KI MOON


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akisalimiana na Balozi Tuvako N. Manongi, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kabla ya kukabidhi hati zake za Utambulisho.
Balozi Tuvako Manongi akimkabidhi Katibu Mkuu Ban Ki Moon hati zake za utambulisho katika hafla iliyofanyika siku ya jumatano ofisini kwa Katibu Mkuu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Balozi Manongi alikuwa kati ya Mabalozi sita waliowasilisha hati zao siku hiyo ya jumatano, ikiwa ni siku chache kabla ya Kuanza kwa Majadiliano ya Mkutano wa 67 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, mkutano utakaohutubiwa na viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu akiwa na Balozi Manongi mara baada ya kupokea hati hizo za utambulisho.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akiwa katika mazungumzo mafupi na Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi mara baada ya kuwasilisha hati zake. katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu alielezea matumaini yake ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Balozi huyo pamoja na Viongozi wakuu wa Tanzania. Kwa upande wake Balozi Manongi aliwasilisha salamu za Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete alizotumwa kwa Katibu Mkuu, na pia akaahidi kutumia uwezo wake wote kutetea maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, pamoja na kushirikiana na Katibu Mkuu katika shughuli za kila siku za Umoja wa Mataifa.

Balozi Tuvako Manongi, akiwa katika picha ya pamoja na maafisa na wafanyakazi wa Ubalozi mara baada ya kuwasilisha hati za Utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. PICHA NA MPIGAPICHA MAALUM

HABARI KAMILI
NA MWANDISHI MAALUM, UN
Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako N. Manongi jana Jumatano amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Balozi Manongi alikuwa kati ya Mabalozi Sita waliowasilisha hati zao siku hiyo ya jumatano ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaowahusisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika Ofisini kwa Katibu Mkuu na kushuhudiwa na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Ubalozini .
Baada ya kukabidhi hati hizo, Katibu Mkuu Ban Ki Moon alifanya mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi.
Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu amesema anaendelea kuitegemea Tanzania kama nchi kiongozi na mshawishi katika kusukuma mbele ajenda zake, zikiwamo zile zinazolenga kufanya mapitio ya baadhi ya majukumu ya Umoja wa Mataifa.
Akasem.“Ninayo mahusiano ya karibu na ushirikiano mzuri sana na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wangu Asha-Rose Migiro. Mimi na wewe tunafahamiana vizuri tumefanya kazi kwa karibu. Ninakutumainia wewe na nchi yako kwamba mtaendelea kuwa msaada kwangu na kushirikiana nami kwa karibu” akasititiza Ban Ki Moon.
Aidha Katibu Mkuu huyo wa UM , ambaye alionyesha wazi kufurahishwa na Uteuzi wa Balozi Manongi kuwa Balozi katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika UM, na hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa mmoja wa maafisa wake waandamizi kabla ya uteuzi huo. Na amemhakikishia Balozi ushirikiano wa karibu na kwamba milango iko wazi wakati wowote akimhitaji.
Kwa upande wake, Balozi Manongi pamoja, na kufikisha kwa Katibu Mkuu Salamu rasmi alizotumwa na Mhe. Rais Jakaya Kikwete amesema, atatumia uzoefu wake kusukuma mbele ajenda si tu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bali pia hasa zile ambazo zina maslahi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika kwa Ujumla.
Sehemu ya salamu rasmi za Mhe. Rais Jakaya Kikwete kwa Ban Ki Moon, zilikuwa ni pamoja na kumshukuru Mkuu huyo wa UM kwa uamuzi wake wa kuitisha mkutano maalum utakaojadili mgogoro na kuzotora kwa usalama na amani katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC).
Mkutano huo utawashirikisha viongozi mbali mbali wakiwamo wakuu wa Nchi na Serikali na wadau wengine kujadiliana ambapo watajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuchagia upatikanaji wa amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano huo utafanyika Septemba 27 hapa Umoja wa Mataifa na unatarajiwa kutoka na tamko rasmi.
Ikumbukwe pia kwamba, Rais Jakaya Kikwete ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) na amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu na amani ya kudumu katika eneo hilo na Mashiriki ya DRC.
Balozi Tuvako Manongi anakuwa Balozi wa kumi na Nne (14) tangu kuanzishwa rasmi kwa Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Mabalozi wengine ambao wamewahi kushika wadhifa huo huko nyuma, ni Balozi Vedast K. Kyruzi, Balozi A.Z. Nsilo Swai, Balozi Chifu Erasto A.M. Mang’enya, Balozi John W.S. Malecela, Balozi Akil B.C. Daniel, Balozi Salim Ahmed Salim, Balozi Paul M. Rupia, Balozi Mohamed Ali Foum, Balozi Dr.Wilbert K. Chagula, Balozi Anthony B. Nyaki, Balozi Daudi N. Mwakawago, Balozi Dr.Augustine P. Mahiga, na Balozi Ombeni Y. Sefue.
Balozi Manongi atafanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano mkubwa na Naibu Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi anayetarajiwa kuwasili kituoni wakati wowote.

No comments:

Post a Comment