Friday, September 7, 2012

MECHI YA NGAO YA JAMII KUCHANGIA HOSPITALI YA TEMEKE


Asilimia tano ya mapato yatakayopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya Simba na Azam yatakwenda kwenye Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
 
Kabla ya kukabidhi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke kupanga maeneo ambayo fedha hizo zitatumika kwenye hospitali hiyo.
 
Mechi hiyo ya uzinduzi rasmi wa msimu wa 2012/2013 itafanyika Jumanne ya Septemba 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
 
Viingilio kwenye mchezo huo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
 
WACHEZAJI WAWILI WAOMBEWA ITC URENO
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ureno (FPF) limetuma maombi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupatia Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wawili waliokuwa wakicheza mpira nchini.
 
Wachezaji wanaoombewa ITC ni Hamis Thabit Mohamed (19) ambaye klabu yake ya mwisho aliyoichezea nchini ilikuwa African Lyon wakati mwingine ni Abuu Ubwa Zuberi (20) ambaye msimu uliopita alikuwa akiichezea timu ya Yanga.
 
Kwa mujibu wa FPF, wote wawili wanaoombewa ITC kama wachezaji wa ridhaa (amateur) ili waweze kujiunga na timu ya Atletico Sport Clube ya Ureno ambayo hata hivyo haikuelezwa iko daraja gani nchini humo.
 
Pia FPF imeombwa kupatiwa hati ya maelezo ya mchezaji (player’s passport) kwa kila mmoja ikiwemo taarifa za ushiriki wao katika mechi rasmi zinazotambuliwa na TFF wakiwa katika klabu zao hizo za zamani.

No comments:

Post a Comment