Sunday, September 16, 2012

MTANZANIA RAJABU MAOJA APANIA KUMCHAPA MNAMIBIA


Bondia wa kimataifa wa Namibia Gottlieb Ndokosho (kushoto) akiwa katika moja ya mapambano yake. Ndokosho anatarajia kupanda ulingoni jijini Windhoek, kupambana na Mtanzania Rajabu Maoja kuwania ubingwa wa IBF

Na Elizabeth John

BONDIA Rajabu Maoja amejinadi kuhakikisha anarudi na ushindi katika pambano lake na ubingwa wa IBF dhidi ya Mnamibia, Gottlieb Ndokosho katika pambano  linalotarajiwa kufanyika Septemba 29, mwaka huu katika jiji la Windhoek, Namibia.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa mkoani Tanga, alikoweka kambi, Maoja alisema, katika pambano hilo lililopewa jina la ‘Vita ya jangwa la Kalahari’ amejipanga kuhakikisha anawapa raha Watanzania kwa kurudi na ubingwa kwani ana imani atarudi nao.

“Nipo huku Tanga ambapo ndiyo nyumbani lakini pia ndipo nilipoweka kambi yangu hadi siku nitakayokwenda katika shindano, nimejipanga kuhakikisha nanyakua ubingwa ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi kwani rekodi yangu ni nzuri tofauti nay a mpinzani wangu na nimejiandaa vizuri kipindi chote tangu nipate taarifa ya pambano hili,” alisema.

Pambano hilo litasimamiwa na rais wa IBF katika Bara la Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabuni na Ghuba ya Uajemi, Onesmo Ngowi huku akishirikiana na Bodi ya Ngumi na Mieleka ya Namibia.

Kwa upande wake Ngowi alisema, mapambano hayo yanatambuliwa na IBF yapo katika mpango wa programu ya ‘Utalii wa michezo’ ambao IBF na USBA umeufadhili na kuuendesha katika bara la Afrika huku Tanzania na Ghana zikiwa ni nchi za majaribio katika mpango huo.

Aliongeza kuwa programu hiyo, itawapa mabondia wengi wa Kitanzania nafasi nyingine ya kugombea mkanda wa IBF sehemu mbalimbali duniani na kuitangaza Tanzania.

No comments:

Post a Comment