Tuesday, September 25, 2012

SIMBA KAMA KAWAIDA, YAICHAPA RUVU SHOOTING 2-1



Mshambuliaji wa Simba, Mrisho Ngasa akimiliki mpira mbele ya beki wa Ruvu Shooting
  Golikipa wa timu ya Ruvu Shooting,  Benjamin Haule akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na beki wa Simba, Shomari Kapombe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba ilishinda 2-1. (Picha na Habari Mseto Blog)
 Mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu akichuana na beki wa Ruvu Shooting
 Shabiki wa Simba
Wachezaji wa Simba wakishangilia bao la kwanza la lililofungwa na Felix Sunzu
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba, wameendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100, baada ya kuibuika na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, pambano lililochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakionekana kupania kuendeleza ubabe kwa timu za Ligi Kuu, Simba ilianza mechi hiyo kwa kusakata soka safi na kushambulia mfululizo, huku safu yake ya mbele ikionekana kuipa wakati mgumu idara ya ulinzi ya Ruvu.
Mfululizo wa mashambulizi ya Simba uliofanywa kwa dakika tofauti na wakali wakali wake Daniel Akuffor, Felix Sunzu, Mrisho Ngasa, uliwalazimu walinzi wa Ruvu Shooting kuelemewa na kufanya madhambi ya mara kwa mara, ambapo beki George Michael alilambwa kadi ya njano dakika ya 23.
Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha, alilazimika kumuonya Michael kwa kadi hiyo, kutokana na rafu aliyomchezea Akuffor, aliyeingia mara kwa mara langoni kwao, ingawa hakuwa makini kutumia mipira ya viungo Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 30, likiwekwa nyavuni na nyota wa kimataifa wa Zambia, Sunzu kwa kichwa maridadi akimalizia krosi iliyopigwa baada ya kazi nzuri ya kuwachambua mabeki iliyofanya na Said Nassor ‘Cholo’ aliyepanda kusaidia mashambulizi.
Dakika 38, Kiemba akawachachafya wachezaji wa Ruvu, kabla ya krosi yake kukosa mmaliziaji na kuishia mikononi mwa Benjamin Haule.
Simba iliendelea kushambulia ambapo katika dakika ya 44, beki Mau Bofu wa Ruvu alimwangusha Sunzu ndani ya 18 na mwamuzi Swai kuamuru ipigwe penati. Akuffor akabeba jukumu la kupiga tuta hilo, ambalo mlinda mlango Haule alipangua na kuwa kona tasa.
Hadi mapumziko, Simba ilitoka ikiongoza kwa bao hilo, huku mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wakishuhudia maamuzi tata ya mwamuzi Swai, aliyeonekana dhahiri kutowajali vibendera wake Samwel Mpenzu na Godfrey Kihwili wote wa Arusha pindi wanapoashiria madhambi.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kushambulia lango la Wekundu na kama si umakini mdogo miongoni mwa washambuliaji wake Paul Ndauka, Hussein Said na Hassan Dilunga aliyekuwa akipenya kirahisi safu ya ulinzi, wangeweza kupata mabao.
Sunzu akafanya shambuliazi kali dakika ya 55 lililotokana na jitihada binafsi akiwalima chenga mabeki, kabla ya Ruvu nao kurudi langoni mwa Simba na Dilunga (Hassani) nusura aipatie bao timu yake, kabla ya mawasiliano madogo na Abdulrahman Mussa kumgharimu.
Ruvu ikapata bao la kusawazisha mnamo dakika ya 78, lililowekwa nyavuni na mtokea benchi Seif Rashid, akitumia makosa ya beki Juma Nyoso wa Simba, aliyeshindwa kuondoa hatari langoni akiwa peke yake na kuukanyaga mpira huo na kuteleza, ambapo Seif aliunasa na kumchambua Juma Kaseja.
Wakati wengi wakimiani matokeo ya pambano hilo yangebaki kuwa ni sare ya bao 1-1, mtokea benchi wa Simba, Christopher Edward aliyeingia kuchukua nafasi ya Akuffor, akaipatia timu yake bao la pili dakika ya 87 kwa shuti na kuamsha mamia ya mashabiki wake jukwaani.
Katika mechi hiyo, Simba ilionekana kutawala mchezo, lakini umakini mdogo mbele ya lango alionao mshambuliaji aliyesifiwa sana kabla ya kunza ligi hii, Akuffor ukaendelea kuzua maswali, kabla ya baadhi yao kulaumu kwa kumchelewesha Christopher, yoso aliyewapa ushindi huo.
Vikosi, Simba; Juma Kaseja, Nassor Cholo, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Amri Kiemba/Koman Keita, Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Chombo/Haruna Moshi, Felix Sunzu, Daniel Akuffor/Christopher Edward na Mrisho Ngasa.
Ruvu Shooting; Benjamini Haule, Michael Pius, Mau Bofu, George Michael, Said Suzan, Gideon David, Abdulrahman Mussa, Hassan Dilunga, Paul Ndauka/Seif Rashidi, Hussein Said na Said Dilunga.
Kutoka Tanga, mwandishi Ahmed Khatib anaripoti kuwa, Mgambo JKT imeshindwa kutumia vema dimba la nyumbani la Mkwakwani jijini humo, baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar, shukrani kwa bao la Kamana Salum, dakika ya 63.

No comments:

Post a Comment