Tuesday, September 25, 2012

MBABE WA WLADIMIR KLITSCHKO AUAWA KWA RISASI



PRETORIA, Afrika Kusini
BINGWA wa zamani wa dunia wa uzani wa ‘heavyweight’ Corrie Sanders amefariki dunia baada ya kupigwa risasi katika tukio la ujambazi lililohusisha matumizi ya risasi za moto jijini hapa.
Mkali huyo mwenye miaka 46, aliripotiwa kuhudhuria sherehe ya kifamilia kwenye mgahawa mmoja jirani na hapa Pretoria katika nchi yake ya asili ya Afrika Kusini, ambapo shambulio hilo lilichukua uhai wake akiwa hospitalini kwa matibabu.
Sanders anakumbukwa zama zake ulingoni, alikotisha kiasi cha kutwaa mataji makubwa ya dunia, likiwamo la WBO ‘heavyweight’ alilotwaa kwa kumchapa Wladimir Klitschko mwaka 2003.
Miaka mitano baada ya ubingwa huo, Sanders akatundika glovu zake mwaka 2008, akiwa na rekodi ya kushinda mapambano yake 42 kati ya 46 aliyopanda ulingoni kupigana.
Sanders akiwa na mkanda wake huo wa WBO Desemba mwaka huo huo wa 2003 apanda ulingoni dhidi ya ndugu yake na Wladimir, Vitali kuwania ubingwa wa WBC  aliokuwa akiushikilia Vitali raia wa Ukraine.
Lakini katika pambano hilo, Sanders alishindwa kurejea kile alichomfanyia Wladimir, baada ya kukubali kichapo cha raundi ya nane ya kwenye Ukumbi wa Staples Center jijini Los Angeles.
Sanders akastaafu masumbwi Desemba 2004 baada ya kumchapa Alexei Varakin katika raubndi ya pili ya pambano lao nchini Austria, lakini akarejea tena ulingoni miaka miwili baadaye.
Februari 2008, Sanders akapoteza pambano lake la mwisho alilotangaza kustaafia, dhidi ya Osbourne Machimana, kuwania ubingwa wa Afrika Kusini ‘heavyweight’ na kumfanya astaafu kwa kichapo.

No comments:

Post a Comment