Tuesday, September 11, 2012

WAONGOZA FILAMU WAPIGWA MSASA


Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo
Na Aron Msigwa – MAELEZO.

Dar es salaam.

 Waongoza filamu nchini wametakiwa kujiendeleza kielimu, kufuata sheria na taratibu zinazosimamia tasnia hiyo ili waweze kuondoa tatizo la kukosekana kwa maadili na weledi katika kazi wanazozifanya.

Akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo  siku 10 yaliyowahusisha wadau kutoka Chama cha  Waongozaji wa Filamu (TAFIDA) takribani 50 yaliyoandaliwa na Bodi ya Filamu  na kutolewa na watalaam kutoka Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo amesema kuwa waongoza filamu wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa filamu zinazotolewa nchini zinazingatia maadili licha ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayoikumba dunia.

Amesema kuwa tasnia ya Filamu nchini  Tanzania  inaendelea kukua kwa kasi kutokana na na kuwepo kwa utandawazi na ukuaji wa teknolojia ambao umewawezesha wadau wa tasnia ya Filamu kupiga hatua katika utengenezaji, uongozaji, uingizaji na usambazaji wa filamu ndani na nje ya nchi.

Bw. Thadeo ameongeza kuwa  kukua kwa soko na ajira miongoni mwa vijana katika tasnia ya Filamu nchini kumeongeza wigo kwa vijana wengi kuingia katika tasnia ya filamu licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hiyo ikiwemo kukosekana kwa weledi, taaluma na maadili.

“Ingawa tumethubutu natambua kuwa soko la ajira kutokana na filamu miongoni mwa vijana na makundi mengine limekuwa sana  ingawa zipo filamu nyingi zinazozalishwa nchini zinazokabiliwa na changamoto ya kukosa weledi, taaluma na maadili”

Amesema kuwa mafunzo hayo yaliyotolewa na wataalam hao kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam ni sehemu ya juhudi za serikali katika kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya Filamu nchini na kupunguza tatizo la maadili katika filamu zinazozalishwa nchini.

“Ni ukweli usiopingika watanzania wengi wanalalamikia hali hii ya athari hasi zinazotokana na mmonyoko wa maadili unaosababishwa na baadhi ya filamu zinazozalishwa nchini ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtakuwa mfano katika kuandaa filamu zenye weledi” amesema Bw. Thadeo.

Kwa upande wake Katibu mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo amewataka waongozaji wa Filamu walioshiriki mafunzo hayo wawe wabunifu na wenye kupenda kujifunza ili waweze kuboresha kazi zao huku  akiwasisitiza kuzingatia maadili ya kazi wanazozifanya.

Pia amewataka washiriki hao waache kulalamika na kutumia muda mwingi kuzijua sheria na taratibu zinazoongoza tasnia ya filamu nchini ili waweze kunufaika na kazi wanazozifanya kwa kupata malipo stahiki ya kazi zao.

“Bodi ya Filamu tumekuwa tukitoa ushirikiano mkubwa kwa wadau wa tasnia ya filamu nchini na pia katika kufanikisha mafunzo mbalimbali na kuwasisitiza wadau kuhakikisha kuwa miswaada na filamu zenu zinapitiwa na kupewa madaraja kwa mujibu wa sheria” amesema.

Naye mtaalam kutoka Idara ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambaye alishiriki kutoa mada mbalimbali katika mafunzo hayo ya siku 10 Dkt. Mona Mwakalinga ametoa wito kwa waongoza Filamu hao kutumia mafunzo hayo kuibadilisha tasnia ya filamu nchini kutokana na mambo ya msingi waliyowafundisha wadau hao.

Mafunzo hayo siku 10 ambayo ni  ya tatu kutolewa yamehitimishwa na utoajia wav yeti kwa wahitimu  yameandaliwa na Bodi ya Filamu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na kuwahusisha washiriki 50 kutoka Chama cha Waongoza Filamu Tanzania (TAFIDA) na wataalam kutoka Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment