Saturday, October 13, 2012

KONYAGI WAPONGEZWA BONANZA LA UJIRANI MWEMA



 Wenyeji wa Bonanza la Ujirani Mwema, Klabu ya Msakuzi Family ya Mbezi, ikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuwavaa Mshikamano Veterani
 Wachezaji wa Msakuzi Veterani (rangi ya Orange) na Mshikamano Veteran (Nyekundu) wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya mechi yao.
 Watu wazima (veterani) walionesha uwezo na vipaji vya hali ya juu katika Bonanza la Ujirani Mwema, liliandaliwa na Msakuzi Family na kudhaminiwa na Tanzania Distilleries Limited kupitia bia ya Konyagi.
 Mmoja wa wadau walioshiriki Bonanza la Ujirani Mwema, akionesha umahiri wake katika kuuchezea mpira. Hakika ilikuwa burudani ya aina yake.
 Kiluvya Veterani katika picha ya pamoja kabla ya moja ya mechi zao katika Bonanza la Ujirani Mwema mchana wa leo.
 Mchuano ulikuwa wa aina yake. Hapa ni mshambuliaji wa Msakuzi Veterani Martini Marela (wa pili kulia) akiwa katika harakati kwenye mechi dhidi ya Mshikamano Veterani.
Kikosi cha Mshikamano Veterani, kabla ya kuwavaa Msakuzi Veterani katika Bonanza la Ujirani Mwema.
Na Salum Mkandemba
UONGOZI wa klabu ya Msakuzi Family ya Mbezi, wilayani Kinondoni, umeipongeza Kampuni ya Tanzania Distilleries Limited (TDL) kupitia bia ya Konyagi, kwa kufanikisha Bonanza la Ujirani Mwema lililofanyika leo kwenye Uwanja wa Mbezi Msakuzi.
Akizungumza na Tanzania Daima wakati wa bonanza hilo, Makamu Mwenyekiti wa Msakuzi Family, Zakaria Nkya, alisema kuwa, TDL kupitia Konyagi ililipamba vema tukio hilo lililovuta hisia za wakazi wengi wa maeneo hayo, huku likishirikisha michezo tofauti kwa vijana na wazee.
Zakaria akabainisha kuwa, lengo la bonanza hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa: “Tumefurahishwa na walivyotufadhili na kufanikisha kufanyika, lakini pia tungeomba wasiishie hapa tu, waende mbali zaidi kwa kukubali kutufadhili tena tukiandaa, lakini pia iwafikie wengi zaidi ya Msakuzi.”
Alisema kuwa, nia ya bonanza hilo lililoshirikisha timu nane za soka, pamoja na michezo ya Netiboli, wavu, kukimbiza kuku na mbio za magunia, lilikuwa ni kuimarisha ujirani mwema baina yao na majirani zao Kiluvya, Temboni na Mshikamano, lakini pia kuimarisha afya miongoni mwa washiriki.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa TDL, Sanki Mbuja, alikiri kufurahishwa na mwamko uliooneshwa na washiriki wa bonanza hilo, na kuwataka kuendelea na mazoezi ya mara kwa mara ili kuimarisha afya zao na kuwa na bonanza lenye ushindani pindi watakapoandaa tena tukio kama hilo.
Katika tamasha hilo, Wakorintho Veterani walifungua kwa ushindi wa penati 4-3 upande wa soka dhidi ya Kiluvya Veterani, penati za washindi zikifungwa na David Edwin Kulwa Mgungusi, Deo Sebastian na Enea Boniface.
Katika mechi nyingine, wenyeji wa bonanza hilo Msakuzi Veterani, walifungwa kwa penati 3-1 baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Mshikamano Veterani, wafungaji wa Mshikamano walikuwa ni Castor Patrick, Victor Kidedea na Brown Mbuta, huku ile ya Msakuzi ikiwekwa nyavuni na Ali Athanas.
Mshambuliaji Atakiwi Omar ‘Mzaramo,’ alifunga bao pekee kwa Kiluvya Veterani na kushinda 1-0 dhidi ya Temboni. Kivutio katika bonanza hilo lililoshuhudiwa na mashabiki kibao, yalikuwa ni matangazo ya moja kwa moja kutoka kwa watangazaji wa kike walio chini ya TDL.

No comments:

Post a Comment