Saturday, October 13, 2012

PEP GUARDIOLA MBIONI KUTUA AC MILAN



MILAN, Italia
Rais wa Milan, Silvio Berlusconi amemtaka makamu wake kuharakisha mazungumzo na Guardiola kocha wa zamani wa Barcelona, ili kuchukua nafasi ya Massimiliano Allegri klabuni San Siro
KOCHA anayewindwa kwa muda mrefu na Chelsea, Pep Guardiola anajiandaa kukutana na Makamu wa Rais wa AC Milan, Adriano Galliani kujadili mambo muhimu kabla ya kuingia mkataba wa kuinoa klabu hiyo ya Serie A, vyombo vya habari Italia vimefichua.
La Gazzetta dello Sport la hapa, limeripoti kuwa, Rais wa Milan, Silvio Berlusconi amemtaka makamu wake kuzindua rasmi mazungumzo na Guardiola kocha wa zamani wa Barcelona, ili kuchukua nafasi ya Massimiliano Allegri klabuni San Siro.
Guardiola aliamua kutorefusha mkataba wake wa kuinoa Barca, kwa madai kuwa anahitaji ‘kuchaji betri’ yake, na inaaminika kiangazi ikijacho anaweza kurejea rasmi katika jukumu la kuinoa moja klabu barani Ulaya.
Licha ya kuwapo kwa taarifa za mpango wa mazungumzo, vyombo mbalimbali vya habari hapa vimedai kuwa, sio Milan peke yao, kwani Tottenham na Bayern Munich nazo zinamuwania kocha huyo mwenye mafanikio makubwa katika soka duniani.
Mmoja wa rafiki na mtu wa karibu na Guardiola, Carlo Mazzone, ambaye alimnoa Guardiola wakati akichezea Brescia, amesema anaamini Pep, 41, angependa kurudi klabuni hapo kufanya kazi, vinginevyo atachagua kati ya Milan au mahasimu wao Inter.
"Guardiola ana marafiki wengi hapa na kimsingi alikuwa na furaha katika maisha yake ya soka nchini Italia," alisema Mazzone kuuambia mtandao wa MilanNews.it.
"Kama hatochagua kurudi hapa, ni wazi kwamba ataamua kuwa kocha wa moja ya timu kubwa na bora za hapa Italia, ambao zinaweza kuwa ndio kipaumbele chake.
"Acha niseme wazi, tumekuwa tukizungumza mara kadhaa kuhusu soka. Mara zote nimekuwa nikimwambia umuhimu wa kuhakikisha anarejesha mguu wake katika viwanjani. Sisi ni marafiki wa karibu, ingawa siwezi kuingilia maamuzi yake.
"Naamini nitakuwa furahani kama Pep atarejea soka la Italia. Wapi ataenda? Milan au Inter – hakuna chaguo nijualo. Alifanya kazi kwa bidii akiwa Hispania na nilidhani kuwa atakuja hapa, ingawa sikuwa na uhakika wa siku gani, kwa mwaka mmoja au mitano."

No comments:

Post a Comment