Thursday, October 11, 2012

TEGETE AMLIZA BABA YAKE KWAO YANGA IKIZINDUKA KWA 3-1.... MBUYU TWITE NAYE ATUPIA

 

 


Shabiki wa yanga akivalia kofia yenye jina la beki Mbuyu Twite. Twite amefunga goli lake la kwanza leo tangu ajiunge na Yanga katika uhamisho uliojaa mvutano na mahasimu wao Simba.

BAADA ya kipigo kisichotarajiwa cha 1-0 ugenini Kagera, Yanga imefufuka jioni ya leo kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Toto African ya Mwanza huku mshambuliaji Jerryson Tegete akiungana na beki Mbuyu Twite na mshambuliaji Didier Kavumbagu 'kumliza' baba yake mzee John Tegete.

Ushindi huo katika mechi ya raundi ya saba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, umeiinua Yanga hadi katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 11, tano nyuma ya vinara Simba na mbili nyuma ya Azam walio katika nafasi ya pili kwa pointi zao 13. Hata hivyo, Simba ina mechi moja mkononi wakati Azam ina mechi mbili mkononi.

Nyota njema kwa Yanga ilianza kuonekana mapema wakati walipopata goli la kuongoza katika dakika ya pili kupitia kwa Kavumbagu, aliyetumbukiza wavuni mpira wa kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima.

Beki wa kati wa Yanga, Twite, ambaye alikaribia kufunga goli lake la kwanza dhidi ya timu iliyomsajili awali kabla ya kuikacha ya Simba wakati shuti lake lilipogonga besela katika sare ya 1-1 ya watani wa jadi Oktoba 3, alijisajili katika kitabu cha wafungaji wa Ligi Kuu ya Bara baada ya kuifungia goli la pili katika dakika ya 21 kufuatia pasi ya beki mwenzake wa kati Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Dakika tatu kabla ya mapumziko, Toto wangeweza kupunguza goli moja pale mwamuzi Ronald Swai wa Arusha alipoamuru ipigwe penalti baada ya Twite kushika mpira akiwa ndani ya 18, lakini Emmanuel Swita alipiga nje penalti hiyo.

Kosa hilo la Swita lilichangia matokeo ya wakati wa mapumziko yasomeke 2-0.

Toto walirejea kipindi cha pili wakiwa na nguvu mpya na kupata goli katika dakika ya 54 lililofungwa na Mussa Said aliyempiga chenga beki Cannavaro na kumfunga kirahisi kipa wa Yanga, Mghana Yaw Berko.

Wakati mashabiki wa Yanga wakianza kupandwa na presha kwamba huenda Toto wangewazuia tena kuondoka na pointi tatu, Jerryson Tegete ambaye alipewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza, alifunga goli la tatu dhidi ya timu hiyo inayofundishwa na baba yake mzazi, John Tegete, katika dakika ya 68

Mapema katika dakika ya 20, Kavumbangu alikaribia kuiongezea Yanga goli la pili lakini nguzo ya lango iliwaokoa Toto baada ya shuti lake kugonga mlingoti na kutoka nje huku kipa Eric Ngwengwe akiwa hana la kufanya.

Ligi hiyo itaendelea Jumamosi wakati mabingwa Simba watakaposhuka ugenini Mkwakwani, Tanga kuikabili Coastal Union, huku Azam wakiwa wageni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Mtibwa Sugar watawakaribisha Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Mechi nyingine za keshokutwa zitazikutanisha Prisons dhidi ya JKT Oljoro (Sokoine, Mbeya), Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Vikosi vilikuwa;

Toto Africans:

Eric Ngwengwe, Kulwa Aryson, Erick Mulilo, Evarist Maganga/ Eric Kyaruzi (dk.73), Peter Mutabuzi, Hamis Msafiri, Emmanuel Swita, Haruna Athumani/ Suleiman Jingo, Mohammed Hussein, Selemani Kibuta na Mussa Said/ Kheri Mohammed (dk.73).

Yanga:
Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athuman Idd 'Chuji'/ David Luhende (dk.60), Frank Domayo/ Shamte Ally (dk. 60), Nurdin Bakari, Didier Kavumbagu, Jerryson Tegete na Haruna Niyonzima

No comments:

Post a Comment