Saturday, October 20, 2012

YANGA YAICHAPA RUVU SHOOTING 3-2 KIURAIIINIIII

 Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima akimtoka mchezaji wa Ruvu Shooting, Said Dulunga  katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga imeshinda 3-2
 Golikipa wa Ruvu Shooting, Benjamin Haule akiokoa moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake

Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima akiwatoka wachezaji wa Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Yanga imeshinda 3-2. (Picha na Habari Mseto Blog)
Beki wa Ruvu Shooting, George Otei akichuana na mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu


DAR ES SALAAM, Tanzania

MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, jana ilibidi wapigane kufa au kupona ili kutoka na pointi tatu muhimu katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara, ilipovaana na maafande wa Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Ikitoka nyuma kwa mabao mawili, Yanga ilipigana kiume na kufanikiwa kuwalaza maafande hao kwa mabao 3-2 na kujikusanyia pointi zilizowasogeza hadi nafasi ya tatu katika msimamo ikiwa na pointi 14, ikitanguliwa na Azam FC pointi 17 na vinara Simba pointi 18.

Katika mechi hiyo ambayo Yanga ilicheza ikiwa na jezi za Vodacom zenye nembo ya rangi nyeusi, Ruvu ilianza kwa kasi na kujipatia bao la kwanza dakika ya tatu, likifungwa na Seif Abdallah kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo, baada ya mabeki wa Yanga kushindwa kuruka naye hewani.

Wakati ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya Mbuyu Twite na Nadir Haraoub ‘Cannavaro’ ikionekana na kutoelewana, walijikuta wakipachikwa bao la pili mfungaji akiwa huyo huyo dakika ya tisa.

Ni bao lililotokana na mpira mrefu wa mlinda mlango Benjamini Haule, aliyepiga kutokea langoni kwake, baada ya mwamuzi Amon Paul kuamuru ipigwe, akikataa katakata kudanganywa na mshambuliaji Jeryson Tegete, aliyejiangusha kwenye boksi na na kupewa kadi ya njano.

Baada ya mabao hayo, Yanga iliyonekana kukosa uelewano katika safu ya ulinzi, ilijipapatua kusaka mabao na juhudi zao zikazaa matunda dakika ya 20, baada ya mpira wa adhabu ndogo wa beki Mbuyu Twite, kwenda moja kwa moja nyavuni.

Tegete ambaye alipoteza nafasi mbili za wazi za kuisawazishia Yanga dakika ya 30 na 32, alikuja kusawazisha makosa na kuipa Yanga bao la pili dakika ya 35.

Hadi mapumziko, timu zote zilikuwa sare ya mabao 2-2, huku Ruvu Shooting wakionekana kutawala mchezo na kuipa wakati mgumu Yanga.

Dakika ya 63, Didier Kavumbagu aliipatia Yanga bao la ushindi, akimalizia uokoaji mbovu wa Haule.
Ruvu ikacharuka dakika za mwisho na kukosa mabao mawili kunako dakika ya 88 na 90, ambapo piga nikupige langoni mwa Yanga iliishia kugonga mwamba na mpira kuokolewa na kufanya hadi filimbi ya mwisho matokeo kubaki Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Yanga iliwakilishwa na Yaw Berko, Juma Abdul/Juma Seif ‘Kijiko’, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Rashid Gumbo/Shamte Ally, Nurdin Bakar, Haruna Niyonzima, Jeryson Tegete/Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu na David Luhende.

Ruvu Shooting; Benjamin Haule, Michael Aidan, Baraka Jaffari, George Otei/Mangasini Mangasini, Ibrahim Shaaban, Ernest Ernest, Raphael Kyala/Ayoub Kitala, Hassan Dilunga, Seif Abdallah, Abrahman Mussa na Said Dilunga/Kulwa Mobi.

Huko Tanga, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ waliutumia vema Uwanja wa nyumbani, Mkwakwani kwa kuwalaza Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1.

Coastal ilijipatia bao la kwanza dakika ya 9, baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Jabu kugonga besela la kushoto na kujaa nyavuni huku kipa Shabani Kado akiwa hana la kufanya, kabla ya dakika ya 38, Danny Lyanga kupachika la pili kwa shuti kali la takribani mita 40.

Mtibwa ilijibu mapigo na kujipatia bao lake pekee la kufutia machozi dakika ya 40, likifungwa na Salum Swedi na dakika ya 82, Lameck Dayton aliipatia Coastal bao la tatu. Hadi mwamuzi Israel Nkongo anamaliza mpira, Wagosi waliibuka kidedea kwa mabao hayo 3-1.

Ligi hiyo itaendelea leo, kwa vinara wa ligi, Simba kupepetana na maafande wa Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani, JKT Ruvu na Oljoro Chamazi Complex wakati maafande wa Tanzania Prisons watawakaribisha Toto Africans ta Mwanza kwenye Uwanja wa Sokoine

No comments:

Post a Comment