Friday, November 23, 2012

AMA KWELI KUNGURU HAFUGIKI’ MUUMIN MWINJUMA ‘KOCHA WA DUNIA’ AIPA KISOGO TWANGA PEPETA



Muumin Mwinjuma, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhama kwake katika bendi ya Twanga Pepeta na kujiunga na Bendi ya Victoria Sound. Muumini alizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, jana. Leo ameondoka jijini Dar kwenda Kenya kusaka wanamuziki. Katikati ni Meneja wake, Abdulfarid na Mkurugenzi wa Victoria Sound Daniel Denga Mjema.
*******************************

*Asema amehama timu ya Taifa na kujiunga na Timu ya Mchangani, Atimkia Kenya kusaka Vipaji vipya 


MWIMBAJI mahiri na mwenye maneno mengi aliyepata kutamba siku za nyuma akiwa na bendi yake ya Double M, Muumin Mwinjuma , aliyewahi kujizolea sifa lukuki kabla ya bendi hiyo kuzimika na kumfanya kuhaha na kuangukia tena kwa aliyekuwa mawajiri wake wa zamani Asha Baraka, aliyempokea na kumwajiri tena katika kundi la African Stars ‘Twanga Pepeta’, hatimaye mwanamuziki huyo ameihama tena bendi hiyo na kutimkia katika bendi iitwayo, Victoria, ambayo yeye kwa mdomo wake amedai kuwa ‘eti’ haitambuliki hata na watu 20.

Muumin, alijiunga na Twanga siku za hivi karibuni na kurekodi wimbo mmoja na bendi hiyo, na sasa amesema ameamua kujiengua katika timu ya ‘Taifa’ na kujiunga na timu ya ‘Mchangani’, yaani amemaanisha kujiengua kwake katika kundi la Twanga na kutimkia Victoria, ni sawa na mchezaji nyota anayegoma kucheza katika kikosi cha timu ya Taifa na kukubari kusajiliwa na timu ya mchangani isiyokuwa na umaarufu.

Akizungumza na mtandao huu wa www.sufianimafoto. Blogspot.com, Kocha huyo amesema kuwa baada ya kutangaza rasmi kuihama bendi ya Twanga, sasa amejipanga kusuka kikosi kamili cha mashambulizi katika bendi yake mpya ya Victoria, ambapo amesema kuwa anaondoka jijini asubuhi hii kuelekea jijini Nairobi, Kenya kwa ajili ya kusaka wanamuziki mahiri na nyota kwa ajili ya kufanya nao kazi katika bendi yake hiyo mpya.

Aidha Muumin, alisema kuwa ameamua kwenda Kenya kusaka wanamuziki kwa sababu antambua kuwa nchini humo, wapo  wanamuziki wengi wakitanzania na wenye vipaji vya hali ya juu,  hivyo ametamani kuwapa shavu hilo ili warejeea nchini kwao na kuonyesha vipaji vyao kwa watanzania wenzao kwama alivyofanya kwa Badi Bakule, Amina Ngaluma, Rashid Mwezingo, Rashid Sumuni, Mohamed Mbale na wengine wengi wakati alipoisuka bendi ya Tam Tam (African Revolution).

“Hakuna mtu aliyekuwa anawajua kina Ngaluma lakini walipotua Bongo kila mtu alikubali moto wao, nitafanya hivyo hivyo katika Victoria Sound” .alisema Muumin 

 “Kama ilivyo kawaida yangu kwani muziki ni kazi yangu, hivyo nawaomba mashabiki wasubiri kuona yale waliyoyamisi kutoka kwangu nikiwa na bendi hii mpya, na wala haitachukua muda mrefu nitakuwa nimekamilisha kikosikazi change na kuwapa raha mashabiki wa muziki wa dansi nchini, Naamini nitafanikiwa kuipandisha chati bendi hii ya Victoria pamoja na kulinda jina na kipaji changu katika tasnia hii ya muziki,” alisema Muumin.

Naye Mkurugenzi wa bendi hiyo, Daniel Denga, alisema kwamba wanajivunia kumpata mwimbaji nyota na mwenye uwezo wa juu katika anga za muziki wa dansi hapa nchini.

“Bendi yetu ilianzishwa tangu mwaka 2007, lakini hatukuweza kufikia muafaka, hivyo naamini sasa malengo yetu yamefanikiwa na yatatimia kwa kutambua uwezo wa Muumini ni mkubwa na hana mpinzani hapa nchini,” alisema Denga.

Muumin amesema atakwenda Nairobi kwa awamu mbili, ya kwanza ni kufanya usajili na ya pili ni kwenda kuwafanyika uhamisho rasmi wanamuziki kutoka Nairobi kuja jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment