Tuesday, November 6, 2012

Kasoro usafiri wa Reli Dar zirekebishwe


Serikali juzi iliweka historia katika nchi yetu baada ya kuzindua usafiri wa treni ya abiria katika Jiji la Dar es Salaam ukitoa huduma kuanzia Pugu Mwakanga hadi Kurasini na Ubungo Maziwa hadi Stesheni katikati ya Jiji. Huduma hiyo ambayo itakuwa ikipatikana asubuhi na jioni Jumatatu hadi Jumamosi inatolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).
   Kwa mara nyingine tunampongeza Waziri Mwakyembe na Serikali kwa jumla kwa kuonyesha ujasiri na uthubutu wa kutenda, kwani suala la kuweka usafiri wa treni ya abiria hapa jijini lilianza kuzungumzwa zaidi ya miaka 30 iliyopita. Hata hivyo, watendaji na wanasiasa walitanguliza mbele nyimbo, mashairi na ngonjera za kukisifu Chama badala ya kubuni mikakati na mipango ya utekelezaji wa mradi huo na mingine mingi ambayo ingesaidia kuinua uchumi na kuwaondoa wananchi katika dimbwi la umaskini wa kutisha.
   Kwa hiyo, msingi wa pongezi zetu kwa Waziri Mwakyembe na Serikali ni utekelezaji wa ndoto hiyo katika muda mfupi tu wa miaka saba ya kipindi cha pili cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Tunasema hivyo kwa kuwa, umuhimu wa usafiri huo wa treni ya abiria jijini ulionekana bayana juzi, pale maelfu ya wananchi, wakiwamo wanafunzi  waliokuwa wamejipanga kandokando ya njia ya reli walipokuwa wakishangilia kwa nguvu kuzinduliwa kwa usafiri huo. Nderemo na vifijo vilisikika na wananchi walisema usafiri huo bila shaka utarahisisha maisha yao na kupunguza msongamano wa magari jijini.
   Tumetiwa moyo na msimamo wa Waziri Mwakyembe ambaye amesema Serikali itahakikisha usafiri huo jijini Dar es Salaam unakuwa endelevu. Pia amezungumzia upanuzi wa usafiri huo katika sehemu nyingine za Jiji siku za usoni. Hizo bila shaka ni salamu tosha kwa wale wenye ndoto za kuuhujumu mradi huo, kwani muda mfupi baada ya Waziri kuzindua safari za treni ya Tazara juzi askari walimtia mbaroni mtu mmoja aliyekutwa akiiba vyuma vya breki vya behewa la treni hiyo.
   Kwa sababu hiyo, tunamshauri Waziri asibweteke, kwani siyo siri kwamba siyo wananchi wote wamefurahishwa na ujio wa usafiri huo wa treni. Tayari baadhi ya wamiliki wa mabasi ya daladala wanalalamika kwamba  mradi huo utawakosesha mapato, hivyo haihitaji elimu ya chuo kikuu kutambua kwamba iwapo watu hao watapata mwanya wa kuuhujumu mradi huo watafanya hivyo.
   Lazima tukumbuke kwamba nchi yetu iliwahi kuwa na vyombo vya usafiri vya umma vilivyokuwa vikifanya kazi kwa ufanisi, vikiwamo Reli ya Kati, Tazara, Kamata, Uda, ATC, Mabasi ya Reli na kadhalika. Lakini vyombo hivyo vilihujumiwa na baadhi ya viongozi serikalini waliokula njama na wafanyabiashara na kuanzisha usafirishaji binafsi wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi ambao tunaushuhudia hivi sasa.
   Ndiyo maana tunamtaka Waziri Mwakyembe asirudi nyuma katika kuhakikisha kwamba mradi huo wa usafiri wa treni unakuwa na ufanisi na hauhujumiwi. Kama alivyokiri mwenyewe, zipo changamoto ambazo zinapaswa zifanyiwe kazi. Kwa mfano, bado matengenezo ya vituo vya kupandisha abiria na vibanda vya tiketi hayajakamilika, kama lilivyo eneo la kupishana treni za TRL lililopo Buguruni ambapo treni moja ilishindwa kufanya kazi juzi.
   Pia bado kuna tatizo la maegesho ya magari ili wenye magari wayahifadhi na kupanda treni kwenda katikati ya Jiji. Tiketi  hazitoshi na wauzaji hawana chenji, hivyo abiria kupata kisingizio cha kusafiri bure. Hii ni mbali na kutokuwapo ulinzi wa kutosha na kanuni na taratibu za kuhakikisha usafiri huo unakuwa wa kistaarabu.
   Ni matumaini yetu kwamba Waziri Mwakyembe ataona umuhimu siyo tu wa kupanua huduma hiyo ya usafiri wa treni kwa sehemu nyingi za Jiji, bali pia atahakikisha huduma hiyo inatolewa kwa wakati wote badala ya asubuhi na jioni kama ilivyo sasa. Tunamtakia kila la kheri.
 

No comments:

Post a Comment