Tuesday, November 13, 2012

LINDI SOCCER ACADEMY YAITAMBIA KINGSTONE NYUMBANI


Mkurugenzi wa Lindi Soccer Academy (LSA), Hafidh Karongo (nyuma), akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa kikosi chake cha LSA kilichoichapa Kingstone ya Kineng'ene, nje kidogo ya Manispaa ya Lindi kwa mabao 3-2, ikiwa sehemu ya maandalizi ya Kombe la Muungano 2012.
LINDI, Tanzania
 
LSA inatarajia kushuka tena kwenye Uwanja wa Mapinduzi Jumapili ijayo Novemba 18, kuumana na wenyeji wengine wa kijiji hicho, Kineng’ene Stars, huku akisema watahakikisha wanawafunga na kuendeleza wimbi la ushindi
KATIKA kujiandaa na michuano ya Muungano Cup 2012 itakayofanyika Desemba huko visiwani Zanzibar, timu ya Lindi Soccer Academy (LSA) ya Lindi Mjini, juzi imeichapa Kingstone ya Kineng’ene nje kidogo ya Manispaa hiyo kwa mabao 3-2.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Mkurugenzi wa LSA, Hafidh Karongo, alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa ni mfululizo wa maandalizi ya kikosi chake, kilichoalikwa kushiriki Kombe la Muungano katikati ya mwezi ujao huko Zanzibar.
Pambano hilo la kirafiki, lilipigwa juzi kwenye Uwanja wa Mapinduzi ulioko katika kijiji cha Kineng’ene, ambapo mabao ya washindi yaliwekwa nyavuni na Mohammed Omari dakika ya tano, Haji Saidi dakika ya 60 na Maximilian Peter dakika ya 63.
Mabao ya wenyeji Kingstone iliyokera mashabiki wake kwa kukubali kichapo hicho kwenye uwanja wa nyumbani, yalifungwa na Fabian Saidi dakika ya tatu na Juma Nungo dakika ya 29 katika pambano kali lililojaa ufundi na ushindani miongoni mwa nyota wa timu hizo.
Karongo aliongeza kuwa, LSA inatarajia kushuka tena kwenye Uwanja wa Mapinduzi Jumapili ijayo Novemba 18, kuumana na wenyeji wengine wa kijiji hicho, Kineng’ene Stars, huku akisema watahakikisha wanawafunga na kuendeleza wimbi la ushindi.
LSA inatarajia kuondoka mjini Lindi mapema mwezi ujao, kupitia jijini Dar es Salaam, ambako watacheza mechi kadhaa za kirafiki – kabla ya kwenda kushiriki Kombe la Muungano huko Zanzibar linalojumuisha timu za bara na visiwani.

No comments:

Post a Comment