Tuesday, December 4, 2012

MWANDISHI TANZANIA DAIMA ATEULIWA OFISA HABARI LINDI SOCCER ACADEMY (LSA)



LINDI, Tanzania
“Uteuzi wake umeanza rasmi Desemba 1 na tunaamini wadau wa LSA watatoa ushirikiano kwake kama Msemaji katika kuhakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo, kwa ustawi wa kituo chetu” 

UONGOZI wa Kituo cha Kuibua na Kuendeleza Vipaji vya Soka Manispaa ya Lindi (Lindi Soccer Academy – LSA), kimemtangaza mwandishi wa habari wa Kampuni ya Free Media Ltd inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Salum Mkandemba (pichani kulia) kuwa Ofisa Habari wa kituo hicho.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa LSA, Hafidh Karongo alisema kuwa, uongozi, wazazi na wachezaji wamekubaliana kwa kauli mmoja kumteua Mkandemba kuwa Msemaji wao, ili kuhakikisha anachangia katika kukiletea maendeleo kituo hicho maarufu Kanda ya Kusini.
Aliongeza kuwa, wao kama LSA wanathamini mchango mkubwa wa mwandishi huyo katika kukitangaza kitu nje ya mipaka ya mkoa na nchi, hali iliyowafanya waamue kurejesha fadhila zao kwa kumpa nafasi hiyo, uteuzi ulioanza rasmi Desemba 1.
“Uteuzi wake umeanza rasmi Desemba 1 na tunaamini wadau wa LSA watatoa ushirikiano kwake kama Msemaji katika kuhakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo,” alisema Mkurugenzi huyo wa kituo hicho maarufu Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Akizungumzia uteuzi huo, Mkandemba alisema kuwa, anawashukuru LSA kwa kutambua mchango wake kiasi cha kuamua kumpa nafasi ya kuwa sehemu ya kituo hicho, huku akiahidi kuhakikisha anatumia nafasi hiyo kukiletea kituo maendeleo ngazi ya mchezaji mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla.
Aidha, lile pambano lililokuwa lipigwe katika kilele cha Siku ya Ukimwi Duniani, Desemba 1 kati ya LSA dhidi ya FC Toto ya Mtwara na kusogezwa mbele kupisha hotuba ya Rais Jakaya Kikwetealiyekuwa mgeni rasmi wa sherehe hizo kitaifa, lilipigwa jana kwenye Uwanja wa Ilulu.
Katika mechi hiyo uliyovuta hisia za wengi, LSA ilikubali kichapo cha mabao 3-2. Wafungaji wa FC Toto katika mechi hiyo walikuwa ni Faraji Namadila, Henry Galus na Ginoa Crispin, huku yale ya LSA yakiwekwa nyavuni na Fabian Said na Abdul Shein.
LSA inajiandaa na mashindano ya Kombe la Muungano, yanayotarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar kuanzia katikati ya mwezi huu, ambapo timu hiyo itasafiri kupitia Dar es Salaam kucheza mechi za kirafiki kadhaa kabla ya Desemba 12 kutua Zanzibar tayari kwa michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment