Sunday, May 5, 2013

DK MWINYI AZINDUA BODI MPYA YA NHIF


 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi (kushoto) akisalimiana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Hamis Mdoe alipowasili kuindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa NHIF, leo kwenye Hoteli ya Courty Yard, Sea View, Dar es Salaam. Wengine ni Mwenyekiti mpya wabodi hiyo, Balozi Ali Mchumo (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba na Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Regina Kikoli.
 Wakurugenzi wa NHIF, wakipiga makofi wakati Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Mwinyi alipokuwa akiingia kuzindua bodi hiyo.
Dk. Mwinyi akihutubia wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo.Kulia ni Mwenyekiti wa bodi hiyo, Balozi Mchumo.
 Baadhi ya mameneja wa Mikoa wa NHIF, na maofisa wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo.
 Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Balozi Mchumo (kushoto) akimshukuru Waziri, Dk. Mwinyi kwa kuzindua bodi hiyo.Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Humba.
 Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba akitoa maelezo kuhusu utendaji wa mfuko huo,  Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikoli
 Mwenyekiti mpya wa Bodi ya NHIF, Balozi Ali Mchumo akuhutubia wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo.
 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi (wa nne kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi mpya ya NHIF. Kutoka kushoto ni Mwanaidi Mtanda,Donnan Mmbando, Mwenyekiti Balozi Ali Mchumo, Mohammed  Hashim, Charles Kajege, Dk. Ali Mohammed na Naibu Katibu Mkuu wa wa wizara hiyo, Regina Kikoli.Waliosimama ni Mkurugenzi Mkuu, Emmanuel Humba (kulia na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Hamis Mdoe.
 Waziri Dk. Hussein Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi pamoja na wakurugenzi wa NHIF.
 Waziri, Dk. Hussein Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mameneja wa NHIF wa mikoa.
 Waziri, Dk. Hussein Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mameneja wa NHIF wa mikoa.
Dk.Mwinyi akibadilishana mawazo na Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Balozi Ali Mchumo (kushoto) pamoja na Mjumbe wa bodi hiyo, Mohammed Hashim.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikoli (kulia) akiagana na Balozi Ali Mchumo. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba. Picha zote na Kamanda wa Matukio)

Na Grace Michael


WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi amesema ni wakati muafaka sasa kwa kuwa na chombo kimoja kitakachokabidhiwa jukumu la kusimamia bima ya afya kwa Watanzania badala ya kushughulikiwa na taasisi nyingi kama ilivyo hivi sasa.


Dk. Mwinyi ameyasema hayo Dar es Salaam leo wakati akizindua bodi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo ameitaka bodi hiyo kuangalia uwezekano wa kuanzisha mjadala wa kuundwa kwa chombo kimoja kitakachosimamia huduma za bima ya afya ili kuwafikia watanzania wote katika utaratibu wa kuchangia kabla ya kuugua.


“Hadi sasa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kusimamia huduma za afya hali inayonishawishi kuwa na chombo kimoja,” alisema Dk. Mwinyi.


Alisema kuwa Serikali inatambua wingi wa mifumo na taasisi zinazojihusisha na huduma za bima ya afya na lengo lililopo ni kuhuishwa ili kuimarisha mfumo wa uchangiaji wa huduma za afya ambapo kwa sasa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekasimiwa mamlaka ya kuendesha Mfuko wa Afya ya Jamii utakaoangalia namna nzuri ya kupanua wigo.


Akizungumzia mchango wa NHIF katika uboreshaji wa huduma za matibabu vituoni, alisema kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na  Mfuko huo angependa kuona Mfuko ukijikita katika uwekezaji unaolenga uboreshaji wa huduma za afya na si vinginevyo, hivyo akaiagiza bodi mpya kuhakikisha inaagalia na kuurejea upya utaratibu wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili watoa huduma wachangamkie zaidi fursa hiyo.


Dk. Mwinyi pia hakusita kuzungumzia mahusiano mazuri ya kazi baina ya bodi, menejimenti na watumishi wa Mfuko ambapo alisema kuwa Mfuko mpaka sasa umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kujenga misingi bora ya uhusiano mwema wa kazi miongoni mwa watendaji wake ambao wamekuwa ni mfano wa kuigwa na taasisi zingine hivyo akasisitiza hali hiyo kuendelezwa ili kuongeza zaidi ufanisi wa utoaji huduma.


Naye Kaimu Mkuu wa Wizara ya Afya, Regina Kikuli aliiambia bodi hiyo kuwa jukumu walilokabidhiwa ni kubwa kwa kuwa linagusa moja kwa moja afya za wanachama na watanzania kwa ujumla hivyo ni vyema bodi ikaliona hilo na kuhakikisha inakuja na mbinu mpya za kuhakikisha inaimarisha na kuboresha Mfuko huo ili uweze kufikisha malengo yake ya kuwahudumia watanzania wote.


Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Balozi Ali Mchumo aliahidi kuwa kazi aliyokabidhiwa kwa kushirikiana na wajumbe wenzake wataifanya kwa uaminifu mkubwa na kwa kutumia uwezo wao wote ili kuhakikisha Mfuko huo unawasaidia watanzania wote.


Akitoa maelezo ya utangulizi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba alisema kuwa moja ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Mfuko kwa sasa ni watanzania wengi kutambua umuhimu wa bima ya afya hivyo Mfuko unafanya kila jitihada ya kuhakikisha inafikia watanzania wengi zaidi na kukabiliana na changamoto zote zilizopo ili lengo la afya bora kwa wote liweze kufikiwa.

No comments:

Post a Comment