Friday, August 16, 2013

Feza Kessy aanika ya Big Brother Africa


 Feza akihojiwa na IK siku alipotolewa BBA
Feza Kessy
     
Na Andrew Chale

“UTAMADUNI wa Kitanzania umenisaidia kuiwakilisha vyema nchi yangu kwenye shindano la Big Brother Africa ‘The Chase’ na kujifunza mengi pia”, hiyo ni kauli ya Feza Kessy wakati wa akijibu maswali ya wandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Feza aliyetua nchini juzi jioni akitokea Afrika Kusini kwenye shindano hilo, ametolewa zikiwa zimebaki siku 14 kumalizika, ambako hivi sasa washiriki saba pekee wamebaki ndani ya Jumba kuchuana ili kuondoka na kitita cha dola 300,000 za Kimarekani,

Anasema, utamaduni huo wa Kitanzania uliomfanya kuweza kukaa kwa siku 77 ndani ya jumba hilo, umeweza kumfanya ajisikie Mtanzania mwenye bahati, kwani aliweza kuvumilia mambo mengi kutoka kwa washiriki wenzake waliotoka nchi zaidi ya 14 barani Afrika, wenye tamaduni tofauti.

Akiendelea kujibu maswali ya wandishi, Feza anakiri kuwa na uhusiano na  Oneal, mshiriki kutoka Botswana, ambaye naye alitolewa wiki moja kabla ya Feza.

“Ni kweli nilikuwa na mahusiano ya kweli na Oneal nilipokuwa ndani ya jumba la Big Brother, zaidi ya hapo ni shindano tu,” anasema Feza.

Hata hivyo, alipoulizwa kama wataendelea na uhusiano nje ya hapo, Feza anasema, ni mapema mno kujibu hilo, kwani amepanga kutulia, kujadili kwa kina suala hilo na kisha atachukua uamuzi.

“Oneal yupo Botswana na mimi nipo Tanzania, sote kwa pamoja hatuna la kusema ila kila mtu anajipanga na litakalotokea tutatoa taarifa,” anasema  Feza na kuongeza.

Anashukuru kwa kuwa mwakilishi wa Tanzania ndani ya shindano hilo na kujiona mtu mwenye bahati.

“Kwanza nashukuru Mungu kuchaguliwa kwangu ndani ya jumba la Big Brother, licha ya kujitokeza wengi mimi ni miongoni mwa washindi, hivyo namshukuru Mungu,” anasema.

Akitoa ushauri kwa vijana, Feza anawataka wasivunjike moyo, zaidi wajitume ili kupambana na maisha ya kila siku na watafikia pale wanapopataka.

MAISHA NDANI YA BBA

Tanzania awali iliingiza washiriki wawili ndani ya jumba hilo, akiwamo  Nando aliyetolewa kwa utovu wa nidhamu na kumuacha Feza ambaye hadi anatolewa alikaa siku 77 pekee.

Kukaa kwake ndani ya jumba hilo, Feza aliweza kuhimili mambo mbalimbali, ikiwemo michezo na kazi zilizokuwa zikitolewa na mkuu wa jumba hilo, Bigg.

Pia, Feza aliwahi kukwaruzana na mshiriki mwenzake, Pokelo wa  Zimbabwe na kusema kuwa, ilikuwa ni sehemu ya mchezo, kwani kila mmoja alikuwa na mambo sawa ya kufanana.

“Sikuchukiana na Pokelo, ukiwa ndani ya jumba lile ni mchezo, kwani mimi na yeye sote tunashabihiana mambo yetu, ikiwemo tarehe za kuzaliwa na sote kwa pamoja tuna mtoto,” anasema Feza.

FEZA AMETOKEA WAPI?

Feza, awali alikuwa mlimbwende na kutwaa taji la Miss Dar City Centre na Miss Ilala mwaka 2005. Licha ya urembo, pia aliingia rasmi kwenye muziki  huku akikiri kupenda muziki hata kabla ya kushiriki shindano la Miss Tanzania.

Feza anasema, alizaliwa mkoani Arusha miaka 25 iliyopita na kupa elimu yake nchini na kisha Uingereza katika mji wa Manchester, ambako pia alipata mtoto wa kiume.

Wimbo wake aliyoutoa awali, aliutoa kwa kushirikiana na msanii Nash, ukienda kwa jina la ‘Strong Woman’.

Feza anasema, anawakubali wasanii mbalimbali nchini, wakiwemo Mwana FA,  TID, marehemu Ngwair, Nurah, Ommy Dimpoz na AY huku ndoto zake kubwa katika muziki ni kufanya kazi kwa pamoja na Rihanna, Lauryn Hill, Tony Braxton na wengine pindi akipata nafasi.

Imeandaliwa na Andrew Chale 0688076376

No comments:

Post a Comment