Friday, August 16, 2013

RT yawaita wadhamini mashindano ya taifa


Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani),  juu masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya mchezo huo, kwenye ukumbi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), jijini Dar es Salaam, juzi. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT, Tullo Chambo na kushoto ni Mwanasheria wa shirikisho hilo, Thabity Bashiri. (Na Mpiga Picha Wetu)

 Na Elizabeth John

"Aidha, aliwashukuru baadhi ya wadhamini wanaoonesha kuanza kuwaunga mkono, ukiwemo Mfuko wa Pensheni wa PPF, TSN Supermarket, Symbion na S S Bakhresa".
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania, (RT), limetoa wito kwa wadau mbalimbali nchini, kuunga mkono jitihada zao za kurejesha hadhi ya mchezo huo nchini, kwa kudhamini matukio mbalimbali yakiwemo mashindano ya taifa yanayotarajia kutimua vumbi, Agosti 23 na 24 mjini Morogoro.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa RT, Anthony Mtaka, alisema, mashindano hayo yamekuwa yakiendeshwa kwa hali ngumu kutokana na kukosa wadhamini hivyo kuchangia kushusha hamasa na viwango vya wanariadha.

Alisema, wanamichezo wasiopungua 450 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wanatarajia kushiriki mashindano hayo makubwa kitaifa, ambayo yatasaidia kuibua vipaji vipya na kwamba, watakaofanya watapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo yale ya vijana huko Mauritius Agosti 29 hadi 31.

Aidha, aliwashukuru baadhi ya wadhamini wanaoonesha kuanza kuwaunga mkono, ukiwemo Mfuko wa Pensheni wa PPF, TSN Supermarket, Symbione na S S Bakhresa.

Katika hatua nyingine, Rais huyo ametaka watu wanaopita mitaani na kutumia mitandao kuichafua RT kutopewa nafasi na vyombo vya habari kwani hawana nia nzuri na maendeleo ya mchezo huo.

Mtaka ambaye amerejea nchini hivi karibuni akitokea Moscow, Russia katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), ulioshirikisha mataifa 206, alisema, moja ya mikakati ambayo ilizungumzwa kwenye mkutano huo ni kuandaa wachezaji wenye ushindani katika mashindano makubwa, hususan Olimpiki na Jumuiya ya Madola.

“Tanzania inawakilishwa na wanariadha wawili katika mashindano ya Dunia ambayo yanaendelea nchini humo, ambapo sisi kama viongozi tumejipanga kupokea matokeo ya aina yoyote kutoka kwao, kutokana na maandalizi wameyafanya,” alisema.

Wanariadha hao ni Msendeki Mohamed na Faustine Mussa ambao leo wanatarajia kupeperusha bendera ya Tanzania katika mbio ndefu za km 42 (Full Marathon)

No comments:

Post a Comment