Tuesday, September 17, 2013

MSANII Prince Ahmed Mgeni hayupo nasi afariki Zenji


Prince Ahmed Mgeni

TASNIA ya sanaa imeendelea kupata misiba baada ya muimbaji nyota wa zamani wa Zanzibar Stars, Prince Ahmed Mgeni kufariki dunia visiwani Zanzibar na jioni hii alitarajiwa kuzikwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka visiwani humo zinasema kuwa, marehemu Mgeni aliyetamba na kuziba nafasi ya Mzee Yusuf alipojiengua katika kundi hilo na kuunda Jahazi, alifariki usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja alipokuwa amelazwa.
Taarifa za awali zinasema marehemu alikuwa akisumbuliwa na kifua kikuu (TB) na kulazwa hospitalini hapo kwa muda mrefu.
Mpaka mauti yalipomkuta jana marehemu Mgeni alikuwa mwanamuziki wa kundi la Zanzibar Njema Taarab.
Kifo cha msanii huyo ni muendelezo wa misiba katika tasnia ya sanaa kuanzia mwishoni mwa mwaka jana ambapo imeshuhudiwa waigizaji na waimbaji wakipoteza uhai kwa sababu mbalimbali ikiwamo ajali na maradhi. Mungu aiweze mahali pema peponi roho ya marehemu Ahmed Mgeni na MICHARAZO inawapa pole familia, ndugu, jamaa na rafiki wa msanii huyo pamoja na wadau wote wa sanaa Tanzania.

No comments:

Post a Comment