LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara inaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi
saba katika viwanja saba tofauti.
Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonalewa na Kocha
Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani
dhidi ya Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa
kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa
na timu hizo.
Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi
iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya
ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi
Simon Mbelwa kutoka Pwani.
Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya
Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio
vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya
Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa
mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na
Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini
Dar es Salaam.
Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye
atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu
ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma
Mwambusi.
Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo
inaendelea kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa
ambayo wikiendi iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini
Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.
No comments:
Post a Comment