Tuesday, September 17, 2013

Tembo Mtoto, nyota iliyozimika ghafla

Bondia Fadhili Awadhi 'Mnyama Chui' kushoto akioneshana uwezo wa kutupiana masumbwi na Yohana Matayo 'Tembo Mtoto' wakati wa uhai wake   mpambano uliofanyika katika ukumbi wa Texas Mnzese Dar es salaam Awadhi alishinda kwa T.K.O ya raundi ya nne Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Na Magendela Hamisi
SEPTEMBA 12 tasnia ya mchezo wa masumbwi ilimpoteza bondia mahili wa uzito wa kilo kilo 66, Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (23), akiwa mazoezini kujindaa na pambano lake la ubingwa wa Taifa dhidi ya Abdallah Mohammed 'Prince Nassib'.
Pambano hilo lilipangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), lilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi.
Bondia huyo mahili ambaye jina lake lilianza kujulikana baada ya kufanya vema katika mapambano yake mengi, tena kwa kushinda kwa KO, wengi walimtabiri mafanikio makubwa kupitia mchezo huo.
Katika vitongoji vya Jiji la Dar es Salaam, hasa kwenye chimbuko la mchezo masumbwi yakiwemo maeneo ya Keko, Manzese, Tandale, Mburahati, Mabibo, Mwananyamala na maeneo mengine hakuna asiyefahamu jina la Tembo Mtoto.
Kwani kabla ya kuanza kushiriki katika ndondi za kulipwa na kuwatwanga mabondia wengi alitokea katika ujenzi wa mchezo huo kwenye ngumi za ridhaa ambako ndiko wanapotokea mabondia bora Tanzania na ulimwengu kwa ujumla.
Prince Nasseb ambaye ndiye anashikilia mkanda wa taifa wa PST, na ndiye alitakiwa kuzitwangwa na Tembo Mtoto,  anasema kifo cha bondia huyo ni pigo kubwa kwake kwani aliamini ndio alikuwa mpinzani wake aliyebaki katika uzito huo wa kilo 66, kutokana na wengi kuwa dhaifu kwake.
"Sikuweza kuamini baada ya kusikia kifo cha mpinzani wangu,  hali ambayo ambayo hadi leo bado inanipa shida kuamini kama ni kweli Tembo Mtoto amefariki, lakini kikubwa ni kumuombea Mungu ampumzishe kwa amani katika makazi ya milele," alisema.
Mratibu wa pambano hilo ambaye ndiye alikuwa kocha wa Tembo Mtoto, Faraji Ndame anasema kifo cha bondia huyo ni pigo katika klabu yake ya Kwame iliyopo Mburahati kutokana na kuw,a kinara wa kusshinda mapambano mengi.
"Ni bondia ambaye alikuwa na namtegemea katika mapambano mengi na siku ambayo anafariki, kwa kweli sikuamini hadi nilipothibitishiwa na daktari wa Hospitali ya Mwananyamala, kwani kabla hajaanguka wakati alipokuwa akifanya mazoezi ya kupiga begi nilikuwa nikimtazama kwa karibu.
"Hadi anaanguka nilikuwa nikimwona, nilipomfuata kumpa huduma ya kwanza alikuwa akitokwa povu na kizuia meno akawa ameking'ata, mdomo ukawa mgumu kufunguka, tulimtoa kizuia meno na kumvua viatu, kisha tukampeleka Hospitali ya Mwananyala, lakini tukaambiwa  amefariki," anasema.
Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa akizungumza na Jambo Leo, kuhusu kifo hicho, alisema wamepokea kwa mshtuko,  lakini kazi ya Mola haina makosa, kinachopaswa kila mmoja kumuombea.
Ninachokifahamu kwa Tembo Mtoto ni kwamba, alikuwa bondia bora mwenye umri mdogo ambaye ndio kwanza alikuwa akiyafuta mafanikio, kwani mapambano mengi aliyocheza alikuwa akishinda kwa KO.
"Katika pambano lake la mwisho ambalo alipigana na Kea Kea alishinda kwa KO, nilikuwa mwamuzi wa mchezo huo, kikubwa ambacho naweza kusema, alikuwa bondia mzuri na atakumbukwa kwa kufanya vema," alisema.
Kocha wa kimataifa wa mchezo huo, Rajabu Mhamila 'Super D', anasema kifo cha Tembo Mtoto ni pigo kubwa katika tasnia ya ngumi kutokana na bondia huyo kuonesha kila dalili za mafanikio katika mapambano yake mengi.
"Kifo cha Tembo Mtoto, hakika kimenishtua kwani ni bondia niliyekuwa nikimfahamu tangu akiwa katika ridhaa, alikuwa akifuata ushauri kwangu," alisema.
"Alikuwa akiupenda mchezo husika, aliuheshimu, aliuthamini kama sehemu ya kazi yake, huku akifanya  mazoezi ya kutosha na kuuthamini mchango wake," anasema Super D.
Dk. Kulwa Killaga ambaye mara nyingi huwapima mabondia kabla ya mapambano, anasema kifo cha Tembo Mtoto kimemshtua, hasa baada ya kukubaliana mambo mbalimbali.
"Nilipozungumza naye mara ya mwisho, aliniomba niwe meneja wake, nikamshauri awe mbali na vitu vilivyo kinyume na maadili ya mchezo wa ngumi kwa lengo la kuepuka athari zinazoweza kujitokeza," anasema.
Anasema kuwa, mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu waratibu kuwapiganisha mabondia bila kufuata utaratibu wa muda wa pambano hadi pambano, madhara yake ni vifo.
"Mfano bondia kapigana wiki moja au mbili, kabla hajafikisha miezi mitatu anapigana tena, hali hiyo ni mbaya sana," anasema.
Anasema kuwa, waratibu wanatakiwa kudhibitiwa katika hilo ili kulinda maisha ya mabondia ambao wengi wao hawana elimu ya kutosha katika hilo na ndicho kinachowagharimu wengi. Pia, anawataka waachane na utumiaji wa bangi.
"Bangi ni kitu kingine kibaya kinachosababisha vifo kwa mabondia, hivyo wadau wa mchezo huo wanatakiwa kuwashauri mabondia wanaotumia madawa ya kulevya," anasema.
Bondia Fadhili Awadhi wa klabu ya Jitegemee, aliyewahi kutwangana na Tembo Mtoto, mwanzoni mwa mwaka huu, alisema kifo cha mwanamasumbwi huyo kimemhuzunisha.
"Niliwahi kupanda ulingoni na marehemu Tembo Mtoto enzi za uhai wake, nikamshinda kwa KO katika raundi ya nne, kifo chake kinanipa majonzi na wakati mwingine nashindwa kuamini," alisema.
Rekodi ya bondia huyo alipigana mapambano saba ya ngumi za kulipwa, alishinda mara nne na kupigwa mara moja na  kutoka sare mara mbili.
Tembo Mtoto alijiunga na ngumi za kulipwa mwaka 2011, akianza safari yake ya masumbwi kutwangana na Seba Temba wa Morogoro, pambano lingine lilikuwa Agosti na kufanikiwa kumtwanga Shujaa Keakea kwa TKO.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amin

No comments:

Post a Comment