Tuesday, October 22, 2013

KIPATO HULETA MAJIVUNO!, USHINDI WA 5-2, 4-1 WAWAVIMBISHA KICHWA MTIBWA SUGAR, WATAMBA KUREJESHA HESHIMA YAO YA NYUMA LIGI KUU


11.Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam

MABINGWA wa zamani mara mbili mfululuizo wa ligi kuu Tanzania mnamo mwaka 1999 na 2000, wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar wametamba kuendeleza vipigo ligi kuu kama walivyofanya mechi mbili zilizopita kwa lengo la kurejesha heshima yao.

Afisa habari wa klabu hiyo, Tobias Kifaru Lugalambwike  imepiga stori na mtandao wa FULLSHANGWE na kueleza kuwa kipigo walichotoa kwa JKT Oljoro cha mabao 5-2 na 4-1 kwa Mgambo JKT ni kiashirio cha kurejea mchezoni na sasa mipango ni kufanya maandalizi ili kuendeleza dozi zaidi kwa timu za ligi kuu.

“Ligi ya msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa, tulianza vibaya na watu wakajua Mtibwa hawana lolote, salamu zetu!, tulikuwa tunazisoma timu na imetuchukua muda kidogo kuzijua, sasa tumeshawapikia dawa yao na ndio maana umeona vipigo hivyo tulivyotoa hapa Manungu”. Alitamba Kifaru.

Afisa habari huyo alisema miaka ya 1999 na 2000 Mtibwa Sugar ilizishinda Simba na Yanga na timu nyingine na kubeba kombe, sasa imefika wakati wa kurejesha heshima yao licha ya kuwepo timu mpya zinazotisha kwa sasa.

“Hizi timu za Azam fc, Mbeya City hazifikia ubora wa Mtibwa na ukongwe wake, tumekuwepo kwenye ligi kwa zaidi ya miaka 20, unapozungumzia timu za ligi kuu zenye historia nzuri unataja Simba, Yanga na Mtibwa, kwa waliozaliwa miaka ya karibuni hawatutambui makali, tuko ngangari kinoma”. Alisema Kifaru.

Kifaru aliongeza kuwa kwa sasa wanajiandaa na mechi ya Octoba 28 mwaka huu katika dimba la CCM Mkwakwani jijini Tanga dhidi ya wagosi wa Kaya, Coastal union, huku lengo lao likiwa ni kuendelea kuzoa pointi tatu muhimu.

“Kocha wetu Mecky Mexime anaendelea kunoa wembe wa vijana wetu, Coastal hawatupi shida sana, tunawaheshimu sana na ikizingatiwa kwa sasa wanafanya vibaya kwani wamepoteza mechi mbili mfulululizo, lakini kwetu lazima waje kukubali kipigo tena”. Alisema kifaru.

Coastal Union walisajili wachezaji wakali lakini siku za hivi karibuni wamekuwa wakiambulia matokeao mabaya, na mechi mbili zilizopita walifungwa 2-1 na Ashanti United na wikiendi iliyopita wakala 1-0 dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba dimba la Kaitaba.

Baadhi ya nyota waliosajiliwa na Coastal Unioni ni pamoja na Haruna Moshi `Boban` , Juma Nyoso, Crispine Odula Wadenya, Kata Yayo, Keneth Masumbuko, na wengineo.

Mtibwa wao wataingia katika mchezo huo wakichekelea, kwani mechi mbili zilizopita walimtafuna JKT Oljoro 5-2 na wikiendi iliyopita wakamfumua Mgambo JKT mabao 4-1.

No comments:

Post a Comment