Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Rufunga akipanda tanki la maji linalosambaza
maji ya Ziwa Viktoria katika miji ya Shinyanga na Kahama,mbele yake
akiongozwa na Mkurugenzi wa KASHWASA Ndg.Kivegaro.
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya kusambaza maji Kahama na Shinyanga(KASHWASA), Ndg.Clement
Kivegaro akiwaonesha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa
Shinyanga chanzo cha Maji kilichopo ziwani ambacho ni "Open channel"
kutoka ziwa Viktoria.kamati hiyo ilitembelea chanzo hicho Jumatatu hii
huko Ihelele wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza.
Wajumbe
wa Kamati ya Ulinzi na usalama wakiendelea kuona kazi zinazofanyika ili
kuhakikisha wananchi wanaopata maji kutoka chanzo hicho yanakuwa salama
kwa matumizi.
Na Magdalena Nkulu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga
MAMLAKA
ya kusambaza Maji katika miji ya Shinyanga na Kahama (KASHWASA)
inayoendesha mradi mkubwa wa maji ambayo chanzo chake ni Ziwa
Viktoria,ina uwezo wa kusambaza na kusafirisha maji kwa mikoa mitano
kutokana na uwezo mkubwa wa mashine za kusukuma maji pamoja na wingi wa
maji.
Hali
hiyo imebainika baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa
Shinyanga ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa Mhe.Ally N.Rufunga,
kutembelea Ofisi kuu za mamlaka hiyo zilizopo Ihelele wilaya ya Misungwi
na Jumatatu ya wiki hii,kuona shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa
maji kutoka kwenye chanzo cha Ziwa Viktoria.
Changamoto
kubwa iliyobainishwa na Mkurugenzi wa KASHWASA Ndg.Clement Kivegaro
wakati akisoma taarifa ya mamlaka ni uchache wa watumiaji wa maji ambapo
alisema kwa sasa mamlaka inasambaza maji kwa asilimia 13 tu ya uwezo
wake hivyo inalazimika kuwasha pampu moja tu ya kusukuma maji, kati ya
pampu tatu zilizopo.
Kamati
iliweza kutembelea mradi huo kwa muda wa zaidi ya saa 2 na kupata
maelezo ya kina juu ya uendeshaji na usambazaji wa maji,ambapo mradi una
uwezo wa kuzalisha maji kwa kiwango cha "cubic metres" 120,000 kwa
siku.
Mradi
unauza maji kwenye mamlaka ya maji Shinyanga( SHUWASA), mamlaka ya maji
Kahama (KUWASA) na jumla kamati 45 za maji vijijini.
Mhe.Rufunga
wakati akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo amesema, lazima
serikali ihakikishe wilaya ya Kishapu nayo inapata maji ili kupanua
wigo wa watumiaji wa maji, na kuhamasisha mikoa mingine kununua maji
kutoka chanzo hicho kwa sababu pamoja na uwezo mkubwa wa mradi huo,bado
haujatumika ipasavyo kulingana na uwezo wake unaokadiriwa kulisha mikoa
zaidi ya mitano.
Amesema
pia kazi ya serikali ni kutafuta fedha ili kushughulikia matatizo
yaliyo ndani ya uwezo wa Mkoa kama kuweka mazingira mazuri kwa watumishi
wa Mamlaka hiyo kwani chanzo hicho kipo mbali na huduma muhimu kama
hospitali, shule na maeneo ya biashara.
No comments:
Post a Comment