Tuesday, November 19, 2013

BENKI YA EXIM YAWAASA WAZAZI KUWEKA AKIBA KWA AJILI YA WATOTO WAO


Meneja Msaidizi wa Benki ya Exim, Tawi la Clock Tower Ibrahim Ukwaju (katikati) akiwaonyesha hundi wanafunzi wa shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam baada ya wanafunzi wa shule hiyo kutembelea benki ili kujifunza shughuli na huduma mbali mbali zitolewazo na benki hiyo.Kushoto ni wanafunzi wa shule hiyo, Eric Sanga (kushoto) na Mathew Kennedy. 
Meneja Msaidizi Benki ya Exim , Tawi la Clock Tower la Benki ya Exim ya Tanzania, Ibrahim Ukwaju (kushoto) akisisitiza jambo kwa wanafunzi wa shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam baada ya wanafunzi wa shule hiyo kutembelea benki ili kujifunza shughuli na huduma mbali mbali zitolewazo na benki hiyo.
Meneja Msaidizi Benki ya Exim , Tawi la Clock Tower la Benki ya Exim ya Tanzania, Ibrahim Ukwaju (mwenye Fulana ya Bluu) akiwaeleza wanafunzi wa shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam jinsi mashine za kutolea fedha (ATM) zinavyofanyakazi baada ya wanafunzi hao kutembelea benki hiyo jana ili kujifunza shughuli na huduma mbali mbali zitolewazo na benki hiyo. 

Mwandishi Wetu

Benki ya Exim imetoa changamoto kwa wazazi kuunga mkono tabia ya kuweka akiba kwa ajili ya watoto ilikujenga jamii yenye uelewa juu ya masuala ya kifedha katika siku za usoni. 

Meneja msaidizi wa Benki ya Exim ya Tanzania Tawi la Clock Tower Ibrahim Ukwaju alitoa changamoto hiyo jana wakati wa ziara ya mafunzo ya Shule ya Msingi ya Kilakala ambayo ipo chini ya uangalizi wa benki hiyo tangu Agosti 2012 na tayari benki hiyo imesaidia kutatua changamoto mbali mbali katika shule hiyo zikiwemo za upungufu wa madawati na vitabu.

Matembezi hayo katika ofisi za benki hiyo yalilenga kuwapatia wanafunzi wa shule hiyo ya msingi picha halisi ya jinsi gani mabenki yanavyofanyakazi kila siku na huduma zitolewazo.

Ukwaju alisema kuwa jamii yenye uelewa juu ya masuala mbali mbali ya kifedha, hususani vijana ni muhimu katika uchangiaji na ukuaji wa uchumi na katika mfumo wa fedha wa Tanzania kwa ujumla.

 “Inapaswa wazazi kuwajengea watoto wao tabia ya kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadae. Ni wakati muafaka sasa kwa wazazi kufungua akaunti benki kwa ajili ya watoto wao. Jambo zuri ni kwamba benki nyingi nchini ikiwemo Benki ya Exim zimeanzisha bidhaa zinazolenga watoto moja kwa moja.” alisema Ukwaju.

Alisema kuwa Benki ya Exim inamkakati kabambe wa kusimamia na kujenga maendeleo ya watoto kwa baadae na ndiyo maana benki hiyo ilianzisha kwa makusudi akaunti maalum ijulikanayo kama ‘Nyota Saving Plan’ kwa ajili ya watoto.

 “Akaunti hii imeanzishwa kwa makusudi kutatua matatizo ya kifedha wanayoyapata wazazi kama vile kuongezeka kwa gharama za kielimu pamoja na huduma nyingine muhimu. Ili kupambana na gharama za mfumko wa bei, wazazi wanahitajika kutunza fedha na kuwekeza, ” aliongeza.

Naye Mkuu wa shule ya msingi ya Kilakala, Abdul Kutarasa wakati wa hafla alisema ziara hiyo ya wanafunzi wa shule yake katika benki hiyo ilikuwa fursa nzuri kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

 “Hii imekuwa ni fursa nzuri ya kujifunza kwa wanafunzi wengi. Naamini fursa hii itawashawishi wanafunzi kusoma kwa bidii zaidi na tunategemea baadhi yao sasa wamepata ushawishi wa kufanya kazi kwenye sekta ya kibenki siku za usoni.

No comments:

Post a Comment