Thursday, November 21, 2013

NGUMI KUPIGWA IJUMAA MOROGORO

Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MAPAMBANO zaidi ya sita ya ngumi za kulipwa yanatarajiwa kufanyika Ijumaa, wiki hii, katika ukumbi wa Yohana Pub ulioko maeneo ya Msamvu, katika Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na mtandao huu, msemaji wa mapambano hayo ambayo awali yalipangwa kufanyika Novemba 24 kabla ya kurudishwa nyuma, Mohamed Jeilan alisema maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba mabondia wote watakaopanda ulingoni wapo katika mazoezi makali.

Jeilan alisema lengo la mapambano hayo yanayosubiriwa kwa hamu kubwa mjini Morogoro, ni kuibua vipaji vya mabondia chipukizi na kuendeleza mchezo huo kiujumla.

Alisema mbali ya mabondia wa Morogoro, mabondia wachache kutoka jijini Dar es Salaam pia wanatarajiwa kualikwa kwa lengo la kutoa changamoto katika mapambano hayo.

“Kimsingi maandalizi yanakwenda vizuri na mabondia wote hivi sasa wanaendelea kujinoa chini ya makocha wao ili kuhakikisha wanafanya vizuri siku hiyo”, alisema.

Msemaji huyo amewataja baadhi ya mabondia watakaopanda ulingoni siku hiyo kuwa ni George Masawe ‘G Mawe’, Athuman Dame, Miraji Abdallah ‘Kinditi One Power’, Salum Saleh ‘Sure Boy’, Beta Kingalu na Ngoda Stopa.

Jeilan ametoa wito kwa mashabiki wa mchezo wa ngumi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya Ijumaa katika ukumbi huo ili kushuhudia mapambano hayo.

“Mapambano yatakuwa makali sana na yenye upinzani wa hali ya juu hivyo napenda kutoa wito kwa mashabiki wa ngumi kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia jinsi gani ngumi zinavyopigwa”, alisema

No comments:

Post a Comment