Mama Maria Nyerere amezungumza na vyombo vya habari nyumbani kwake Msasani, na kuwataka vijana waliokwenda kumtembelea kuzunguka nchi mzima kuwaambia ukweli watanzania juu ya Maisha halisi ya mwalimu na mchango wake katika ujenzi wa Taifa huru la Tanzania.
Vijana
wazalendo na wapenda Amani ambao wamemtembea Mama Maria wakiongozwa na
Kiongozi wao anayejulikana kwa Jina la Mohamed Nyundo, wamesema wako
pamoja na familia hiyo na kwamba wamesikitishwa na kampeni inayoendelea
ya kumchafua Baba wa Taifa, kumkebehi na kumtuhumu kwa Uzushi na
uzandiki.
UJUMBE WA VIJANA KULAANI VITENDO VIOVU VYA KUMVUNJIA HESHIMA BABA WA TAIFA.
Kumekuwepo
na kampeni yenye nia ovu iliyoasisiwa hivi karibuni ya kuharibu taswira
na heshima ya Baba wa Taifa Mwalimu Kambarage Nyerere katika jamii ya
kitanzania na kimataifa. Kampeni hiyo inayoendeshwa na vibaraka wa nchi
za magharibi na Ulaya, wazandiki na maadui wa Amani ya Tanzania
imeendelea kusambazwa kwa kasi na kwa gharama kubwa.
Kutokana
na kuwepo kwa Kampeni hiyo, jumuiko la Vijana Wazalendo na wapenda
Amani tumeamua kutoa tamko hili la kulaani na kupinga vitendo viovu vya
baadhi ya watu kumtuhumu, kumkebehi na kumtukana Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Kwa
kutambua Mchango wa Baba wa Taifa kama muasisi wa Taifa hili, mpigania
Uhuru shupavu, Shujaa aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwa watu wake na kwa
kutambua umahiri na jitihada za kujenga Taifa lenye Muungano, Umoja,
Amani na Utulivu, jumuiko la Vijana wazalendo limeamua kuukumbusha Umma
wa watanzania juu ya mchango wa utumishi uliotukuka wa Mwalimu Nyerere
katika ustawi wa Taifa letu, lakini pia kuhamasisha watanzania hasa
Vijana kuenzi kwa Vitendo moyo wa kujituma,weledi na busara za
kiuongozi, pamoja na ushujaa na ushupavu wa Mwalimu Nyerere.
Sisi
Jumuiko la Vijana wazalendo, tumeona ni vyema kuja kumfariji Mama yetu,
Mama Maria Nyerere pamoja na familia nzima ya Mwalimu Nyerere na Kwamba
sisi kama wananchi na Vijana makini tutaendelea kuwa pamoja na familia
katika kupinga na kulaani vitendo hivyo viovu vya kejeli, matusi, tuhuma
na kebehi zinazoelekezwa kwa Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere.
Kwa
masikitiko makubwa, tumeshitushwa na kufadhaika kuona chombo kikubwa na
taasisi muhimu ambayo ni muhimili mkubwa wa Serikali kama Bunge la
Jamhuri la Muungano wa Tanzania linakuwa ndio uwanja wa matusi ya
kumtukana muasisi wa Taifa hili, imetusikitisha na kutufedhehesha.
Imefika wakati sasa,
kwa Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudhibiti na
kuondoa kinga yake kwa wale wote ambao kwa ujinga na kutumika wameamua
kuanzisha na kuendesha kampeni kabambe ya kutia doa taswira na heshima
ya Baba wa Taifa.
Imetolewa na:
Mohamedi Nyundo.
Kiongozi wa Jumuiko la Vijana Wazalendo na Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Pwani.
No comments:
Post a Comment