Tuesday, June 10, 2014

BALOZI MPYA WA MAREKANI AJITAMBULISHA KWA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkaribisha Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzani, Mark Childres, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Juni 9, 2014 kwa mazungumzo na utambulisho wa balozi huyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika mazungumzo na Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childres, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Juni 9, 2014 kwa mazungumzo na utambulisho wa balozi huyo.
*************************************** 
BALOZI MPYA WA MAREKANI AJITAMBULISHA KWA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS
Ikulu, Dar es Salaam: 2014-06-09 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Balozi mpya wa Marekani, Mheshimiwa Balozi Mark Childress ambaye amefika ofisini kwa mheshimiwa Makamu wa Rais kwa ajili ya kujitambulisha.
Balozi Childress alimueleza Mheshimiwa Mkamu wa Rais kuwa, Tanzania ni nchi yenye uhusiano maridhawa na Marekani na kwamba katika kipindi chake kama Balozi atahakikisha uhusiano huu mzuri uliojengwa unadumishwa na kwamba, nchi hizi mbili zinazidi kuwa na maeneo ya kushirikiana hasa yanayolenga kuboresha maisha ya watu na kuwapatia maendeleo.
Balozi Childress pia alisema kuwa Tanzania imekuwa ikitumia kama mfano kufuatia kuonesha mabadiliko ya haraka katika miradi mbalimbali inayoendeshwa hapa nchini kwa ushirikiano na watu wa Marekani na akafafanua kuwa, kazi iliyoko mbele ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua zaidi na sio kurudi nyuma.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, kila nikipata fursa ya kukutana na wenzangu tumekuwa tukizungumzia suala la Tanzania kupiga hatua kwa haraka. Mna mambo mengi yaliyofanyika na kazi iliyopo ni kuendelea kupiga hatua pasipo kurudi nyuma,” alisema.
Kwa upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais alimueleza Balozi Childress kuwa, Tanzania ipo katika kipindi ambacho kinaonesha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kwamba kazi ya serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa uchumi unakuwa na unasaidia vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mtazamo wetu katika serikali ni kuwa Tanzania itapiga hatua kubwa katika miaka michache ijayo. Lengo letu ni kutazama kuwa ukuaji wa uchumi hauwi wa muda mfupi, tunatazama pia maendeleo kwa vizazi vijavyo.
Kuhusu suala la utunzaji mazingira, Balozi Childress alisifu hatua za Mheshimiwa Makamu wa Rais hasa katika kazi ya uhamasishaji upandaji miti na akasema, utunzaji wa mazingira ni jambo la muhimu ili kuifanya nchi yetu iweze kuendelea na isikabiliane na matatizo yanayotokana na mazingira kuharibiwa.
“Nakupongeza Mheshimiwa Makamu kwa kazi yako ya uhamasishaji utunzaji wa Mazingira. Usichoke kufanya hivyo maana unasaidia dunia,” Balozi Childress alisema.
Imetolewa na : Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment