Mwenyekiti
wa wabunge wa Tanzania katika bunge la Afrika Mashariki(EALA) Mh. Adam
Kimbisa akitoa tamko la wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika
Mashariki kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu sakata la
kumvua madaraka spika wa bunge hilo wakati wa Mkutano uliofanyika
katikamukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara
ya Habari(MAELEZO) Bw. Assah Mwambene.
Mbunge wa Tanzania katika bunge la Afrika
Mashariki(EALA) Mh. Twaha Taslima akieleza jambo kwa waandishi wa Habari(Hawapo
pichani)wakati wa Mkutano uliofanyika katikamukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO). Kushoto ni Katibu wa wabunge wa Tanzania katika bunge hilo Mh.
Shy-rose Bhanji.
*************************************
BUNGE LA
AFRIKA MASHARIKI KANDA YA TANZANIA (EALA-TZ)
TAMKO LA
PAMOJA LA WABUNGE WA TANZANIA WANAOWAKILISHA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI (EALA)
JUU YA SAKATA LA KUTAKA KUMVUA MADARAKA SPIKA WA BUNGE HILO 0/06/2014
Sisi, Wabunge saba wa Bunge la Afrika Mashariki
kutoka Tanzania (EALA-TZ), tunapenda kusisitiza msimamo wetu wa kutounga mkono
jaribio la kutaka kumuondoa madarakani Spika wa EALA, Mh. Margaret Nantongo
Zziwa.
Baada ya kutafakari
kwa uangalifu na kwa umakini mkubwa kuhusu chanzo halisi cha hoja yenyewe ya
kutaka kumuondoa Spika wa EALA madarakani, tuligundua mambo yafuatavyo:
1. Hoja hii haina maslahi ya Tanzania na iko
kinyume na malengo ya ushirikiano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Tumebaini kuwa hoja yenyewe ni sehemu ya "mchezo mchafu" wa ajenda ya siri ya kujaribu kuweka mbele
maslahi ya baadhi ya wanachama wachache wa jumuiya badala ya kuzingatia maslahi
mapana ya EAC.
2. Tuhuma mbalimbali zilizotajwa dhidi ya
Spika wa EALA kuhusu yeye kuonesha upendeleaji, ujeuri na mapungufu mengine ya
uongozi zimegundulika kuwa hazina mashiko na wala mantiki .
3. Kitendo ambacho kimetushtua ni kuwa
kumekuwa na majaribio kadhaa ya baadhi ya Wabunge wa EALA kutoka nje ya
Tanzania na viongozi wa Sekretarieti ya EAC kutaka kulazimisha sahihi za baadhi
ya Wabunge wa Tanzania zitumike kinyume na utaratibu kuunga mkongo Azimio tajwa
(kitu ambacho tunakipinga kwa nguvu zote). Hii inadhihirisha kuwepo kwa ajenda ya
siri katika sakata hilo dhidi ya maslahi ya Tanzania na jumuiya kwa ujumla.
4. Kufuatia
malumbano yaliyoibuka katika kikao cha Bunge cha mwezi Machi huko Arusha, sisi
Wabunge wa Tanzania tulipokea maoni na masikitiko mengi kutoka kwa wana Afrika
Mashariki na viongozi kwa ujumla wakitusihi kumaliza tatizo hili kwa njia ya amani
na utulivu, lakini jitihada zetu ziligonga ukuta. Hatua hii ilizidi
kutudhihirisha kuwepo kwa ajenda ya siri.
Ikumbukwe kuwa azimio
la kutaka kumuondoa Spika madarakani awali lilipangiwa kuwasilishwa katika
kikao cha Bunge la EALA cha mwezi Machi 2014 huko Arusha lakini liligonga
mwamba baada ya kuibuka mabishano ya kisheria, hali iliyopelekea kuahirishwa
kwa kikao hicho.
Hoja hii ililetwa
tena kwenye vikao vingine vya EALA, lakini baada ya kutafakari kwa makini
kuhusu chanzo halisi cha mzozo huu, idadi kubwa ya Wabunge kutoka Tanzania (7
kati ya 9) waliamua kwa pamoja kuipinga hoja hii kwani imekosa mashiko na haizingatii
maslahi ya Tanzania na maslahi mapana ya jumuiya kwa ujumla.
Aidha, wabunge
watatu wa EALA kutoka Tanzania ambao awali waliunga mkono hoja hii waliamua baadae
kuipinga kwa kutoa sahihi zao kwa hiari yao wenyewe na walimwandikia barua
Katibu wa Bunge wa EALA kumueleza maamuzi yao kwa mujibu wa utaratibu mnamo
tarehe 29 Mei 2014. Barua hizo za Wabunge wa Tanzania wa EALA kutoa sahihi zao kwenye
hoja hiyo zilipokelewa rasmi na Katibu wa Bunge.
Wabunge hao wa EALA
kutoka Tanzania walitumia haki zao za kikanuni kuondoa sahihi zao kama
inavyoeleza katika kanuni ya 9 (2) ya Kanuni na Utaratibu wa Uendeshaji wa
Bunge (Rules of Procedure of the Assembly) inayosema: "Azimio la kumuondoa
Spika madarakani halina budi kuambatana na sahihi zisizopungua nne kutoka kila
nchi mwanachama."
Hoja yenyewe ya
kumuengua Spika wa EALA ni batili kisheria kwa kuwa haikuwasilishwa Bungeni
ndani ya siku 7 tangu ilipopelekwa kwa Katibu wa Bunge na pia imekosa sahihi za
kuungwa mkono na wabunge wanne kutoka kila nchi mwanachama wa EAC kama kanuni
zinavyotamka.
Uamuzi wa Wabunge wa
EALA kutoka Tanzania kuondoa sahihi zao kwenye hoja hiyo ni lazima uheshimiwe
na kila mtu kwa kuwa wanatekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Tunaomba uongozi wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ngazi zote ikiwemo Sekretarieti ya jumuiya
kuheshimu maamuzi ya Wabunge wa EALA kutoka Tanzania. Ikumbukwe kuwa hapo
awali, wabunge wa 5 wa EALA kutoka Tanzania kati ya jumla ya wabunge wote 9 wa Tanzania
walionesha kuunga mkono hoja hii. Baada ya kubaini kuwepo kwa “mchezo mchafu” na ajenda ya siri,
Wabunge watatu wa EALA kutoka Tanzania waliondoa sahihi zao na hivyo basi
kufanya idadi kubwa ya Wabunge kutoka Tanzania (7 kati ya 9) kuipinga hoja hii
batili.
Wabunge wa EALA
wameshapoteza muda mwingi, fedha na rasilimali nyingine mpaka sasa kwenye hoja
hii isiyo na tija ya kujaribu kumng'oa madarakani Spika wa EALA. Sasa hatuna
budi kuweka jitihada zetu kwenye kazi muhimu ya kutetea maslahi ya raia wapatao
milioni 140 wa Afrika Mashariki.
Hatuwezi kuwahudumia
raia wa Afrika Mashariki kwa kuweka mbele ajenda za siri na kujishughulisha
kwenye siasa za malumbano. Wananchi wa Afrika Mashariki wanataka kuona faida
halisi kutoka kwenye jumuiya yao. Tuna imani na Spika wa sasa wa Bunge la EALA
kuwa ni kiongozi sahihi wa kuongoza Bunge hilo.
Tunaamini kuwa
hakuna tija yoyote kwa Wabunge wa EALA kuendelea kupoteza fedha za walipa kodi
wa Afrika Mashariki kwa kujadili hoja hii batili. Badala yake, Wabunge wa EALA
wana kazi ngumu ya kusimamia maslahi ya wananchi wa jumuiya wanaotaka kupata
elimu bora, maji safi na salama ya kunywa, uhakika wa chakula, afya bora,
miundombinu ya kisasa na maendeleo ya kiuchumi -- siyo siasa za ulaghai.
Tunatoa wito pia kwa
Wabunge wenzetu wa EALA kutoka nchi nyingine wanachama na kwa viongozi wa
Sekreterieti ya EAC kutojihusisha na ajenda zozote za siri za kujaribu kumng'oa
Spika wa sasa wa EALA aliyepo madarakani kisheria. Wananchi wa Afrika Mashariki
wanastahili zaidi ya hayo.
Njia pekee ya
kufikia maslahi yetu ya pamoja ni kwa kutumia ushirikiano, badala ya kuendekeza
malumbano na siasa za chuki na kututenganisha.
Sisi Wabunge saba bado tunasisitizia AMANI NA UTULIVU kwani bila ya
hivyo hakuna maendeleo na ustawi wa jamii.
Tamko hili
limetolewa Dar es Salaam tarehe 9 Juni 2014 na Wabunge wafuatao:
Mhe. Adam Kimbisa,
Mwenyekiti wa Wabunge wa EALA wa Tanzania
Mhe. Shy-rose
Bhanji, Katibu wa Wabunge wa EALA wa Tanzania
Mhe. Charles
Makongoro Nyerere, Mbunge wa EALA
Mhe. Maryam Ussi,
Mbunge wa EALA
Mhe. Bernard
Murunya, Mbunge wa EALA
Mhe. Twaha Taslima,
Mbunge wa EALA
Mhe. Angellah
Kizigha, Mbunge wa EALA
Mwenyekiti, Wabunge wa EALA wa Tanzania
Katibu, Wabunge wa EALA wa Tanzania
Mwanasheria, Wabunge wa EALA wa Tanzania
No comments:
Post a Comment