Wafanyakazi
wa Shirika la Madini la Taifa STAMICO wakiwahudumia wageni
waliotembelea katika banda lao kwenye maonyesho ya wiki ya Utumishi
yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam. Wafanyakazi
wa Shirika la Madini la Taifa wakiangali moja ya majarida ya nayoelezea
shughuli za shirika hilo kutoka kulshoto ni Bibiana Ndumbaro, Denis
Silas na Charles Mawala. Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Shirika la Madini la Taifa STAMICO Bw.
Leornald Mwakalebela akiwapatia majarida wafanyakazi wenzake ili
kuwagawia wananchi wanaotembelea banda hilo.
....................................................................................
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurungenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Madini la Taifa,
Mhandisi Edwin Ngoyani ameahidi neema kwa wachimbaji wadogo wa madini
na vito nchini kwa kuwawezesha kupata masoko ya bidhaa zao pamoja na
kuwapatia zana za kisasa za uchimbaji madini.
"Malengo yangu makuu katika shirika hili ni kuhakikisha
wachimbaji wadogo wanawezeshwa kunufaika na rasilimali za nchi yetu
pamoja na kuhakikisha kwamba STAMICO linatoa mchango wa mapato katika
mfuko mkuu wa hazina kwa kujiendesha kwa faida," Mhandisi Ngonyani
alisema katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa kujiamini, Mhandisi Ngonyani alisema anatarajiwa
malengo yake katika STAMICO yataanza kuzaa matunda ndani ya miaka
miwili mpaka mitatu ijayo.
Akizungumzia mkakati kwa wachimbaji wadogo, Ngonyani
alisema,ndani ya miaka miwili ijayo, shirika hilo litanunua mitambo
miwili ya uchimbaji wa madini ya kisasa (drilling rigs) ambayo
itatumiwa na wachimbaji wadogo.
“Lengo ni kuwafanya wachimbaji wadogo wanufaike na wawe sehemu
ya uwekezaji kwenye rasilimali zao, kama ambavyo hao wawekezaji wa nje
wanavyowekeza, na sasa watanzania nao watawekeza, ila lazima
tuwawezeshe," Ngonyani alisisitiza.
Alisema lengo la STAMICO kwa wachimbaji wadogo ni kuhakikisha
wanawezeshwa kuwekeza na kuchimba kisasa ili pia watoa mitaji ambao ni
benki wawe na uhakika wa fedha zao kurejeshwa, na kwamba hata ikibidi,
shirika hilo litawawekea dhamana ili wawezeshwe kibenki.
Alisema hilo litawezekana baada ya mkakati wao wa kuanzisha na
kuboresha takwimu za wachimbaji wadogo ambazo zitakuwa na taarifa zao
ikiainisha mahali walipo,aina ya madini wanayochimba na mahitaji yao.
Pia mkakati mwingine ni kubaini vyanzo vya migogoro kwenye
maeneo ya wachimbaji na kutafuta suluhu ikiwa ni pamoja na kutenga
maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo ili kuepusha migogoro isiyo ya
lazima.
Katika hatua nyingine, Ngonyani alizungumzia mradi wa uchimbaji
madini kwenye mgodi dhahabu wa Tulawaka ambao hivi sasa umenunuliwa na
shirika hilo na kuitwa Biharamulo unaosimaimamiwa na kampuni ya
StamiGold.
Alifafanua kwamba mgodi huo utaanza kazi rasmi Agosti 8, mwaka
huu na kwamba baada ya miaka miwili na nusu, wanatarajia kupata faida ya
shilingi bilioni saba.
Awali mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na kampuni ya African
Barrick Gold (ABG) na mwishoni mwa mwaka jana STAMICO ikaununua kwa dola
za Marekani milioni tano.
ABG iliuza mgodi huo kutokana na kwamba kiasi cha wakia 100,000
kilichopo katika eneo la mradi ni kidogo kwa uchimbaji mkubwa kwa
kampuni hiyo kubwa ya madini duniani.
"Hata hivyo tuna matumaini kwamba katika eneo la kilometa nne
kutoka kwenye eneo la mradi kuna uwezekano wa kuwapo mashapo ya kati
150,000 mpaka 200,000. Tutaendelea na utafiti katika eneo hili,"
Mhandisi Ngonyani alisema.
Kwa upande wake, Meneja Uchorongaji wa Stamico, Alex Rutagweleka
alisema hivi sasa miradi mitano iko kwenye ubia na shirika hilo kwa
ajili ya uwekezaji na kuitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa
Itetemia mgodi wa dhahabu ambao Stamiko wameingia ubia na Kampuni ya
Madini ya Tancan Ltd.
Mradi mwingine ni wa Buckreef wa dhahabu ulioko Geita ambao
Stamico wameingia ubia na Kampuni tanzu ya TANZAM 2000, ambapo Stamico
wana hisa asilimia 45 na 55 iko kwa kampuni hiyo na kwamba wanategemea
uzajishaji utaanza Novemba mwama huu.
Aidha mradi mwingine ni Kiwira ambao unazalisha makaa ya mawe kwa ajili ya kufua umeme utakaounganishwa kwenye gridi ya taifa.
Akizungumzia mradi huo,Meneja fedha na Utawala wa Stamico, Peter
Gembe alisema lengo la mradi huo ni kufua megawati 200 za umeme kwa
ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya taifa kutoka kwa kiwango cha awali
cha megawati 6.
Stamico ni shirika la umma lililoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo
la kuongeza mchango wa sekta ya madni katika pato la taifa na kuzalisha
nafasi za ajira kwa watanzania.
No comments:
Post a Comment