Mkuu wa Kitengo cha Usuluishi na Ushauri wa Sheria (katikati)
akisisitiza jambo kwa wanahabari alipokuwa akitoa tamko kwa vyombo vya
habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Valerie Msoka.
Kushoto ni Mwanasheria wa Tamwa, Loyce Gondwe na kulia ni Mwanachama wa
TAMWA, Marie Shaba. Mkutano wa waandishi wa habari pamoja na wawakilishi wa TAMWA wakisoma tamko lao juu ya umuhimu wa jamii kuwajali watoto.
Mwanachama wa TAMWA, Marie Shaba (wa kwanza kulia) akizungumza katika
semina kwa baadhi ya wanahabari juu ya uandishi wa habari za kuwatetea
watoto.
CHAMA
cha Wanahabari Wanawake nchini Tanzania (TAMWA) kimeitaka Serikali na
jamii kwa ujumla kuwekeza katika kumuandaa mtoto kwani licha ya kuwa
zawadi kubwa, watoto pia ni tumaini na uhai wa taifa kuendelea. Kauli
hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka
katika taarifa iliyosomwa kwa wanahabari jijini Dar es Salaam
kuhamasisha jamii kwa ujumla kuwajali watoto hasa kwenye mchakato
unaoendelea hivi sasa wa uundaji wa Katiba Mpya.
TAMWA
ilisema mabadiliko ya sera za siasa na uchumi kwa kiasi kikubwa
yameathiri namna taasisi za kijadi na kidini zinavyofanya kazi na
kujikuta zikijiondoa kwa namna moja ama nyingine katika suala zima la
kuwasaidia pamoja na kuwalinda watoto.
"...Leo
hii mzigo mkubwa wa malezi umeachiwa Serikali kwa kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na ile ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Wizara ya Ajira na Kazi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, taasisi za
kidini, asasi zisizo za Kiserikali, Televisheni, sinema, wasanii na hata
majambazi nao wanalea watoto," ilisema taarifa hiyo.
Alisema
kwa sasa Wizara nyingi zinaamini hazihusiki na watoto hivyo kujikuta
sera na sheria zao nyingi kuwasahau watoto. Alisema suala la watoto ni
mtambuka hivyo kula kila sababu ya kufanya mabadiliko yoyote ya sera na
sheria kuwa na manufaa zaidi kwa watoto hasa katika kipindi hichi cha
mabadiliko ya katiba. Aliongeza kuwa suala la malezi ya mtoto ni jukumu
la kila mmoja na sio kuwaachia baadhi ya watu tena wawalee watoto hao
wanavyojua wao kwa maslahi yao pekee. Watoto ni zawadi kubwa na tumaini
la taifa kuendelea hivyo kuna kila sababu ya kuwekeza katika kundi hilo.
"...Tujipange
ili tusiendelee kudharauliwa kuwa hatuna uwezo wa kuwapenda na kuwalea
kwa ajili ya ufukara. Ni dhabi kusikia kuwa umemchoma moto mtoto kwa
kuiba shilingi mia kwa ufukara. Au wengine kunajisi watoto wadogo kwa
kisingizio kuwa ufukara ndio umekusababisha utende hayo. Tunasema huo ni
zaidi ya unyama...tuache kuvumilia aina yoyote ya ukatili unaowafanya
watoto wakose furaha, upendo na matumaini," alisema katika taarifa yake.
Mkurugenzi
huyo wa TAMWA alisema zamani enzi za bibi na babu taasisi za jamii
zilisaidia kumtayarisha kijana juu ya nmna ya kuishi na watu, majirani,
wenzi wake huku suala la malezi ya watoto likiwa ni jukumu la jamii
nzima jambo ambalo kwa sasa limekoma baada ya kuingia utandawazi.
Alibainisha kuwa kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza katika dhana
nzima ya malizi kwa watoto hatuwezi kurudia kama ilivyokuwa enzi za
mabibi na mababu bali inaweza kutumika falsafa zao na kujikuta
tunaendelea kuendesha maisha yetu kwa sasa.
Alisema
ipo haja ya kuchambua jinsi gani shule na hata malezi ya nje ya shule
yanavyoweza kuwa pahala pa kunoa na kumpiga msasa mtoto ili afikie umri
wa miaka 18 awe amehitimu, anaheshimu haki zake na za wengine, aweze pia
kuishi kwa kujitegemea na kutumia elimu na ujuzi alioupata kwa faida ya
jamii. Hata hivyo aliitaka jamii kuunga mkono juhudi zote chanya
zinazowekwa ili kujenga mazingira mazuri ya kumfanya mtoto aweze kuishi
kwa amani, furaha, upendo na matumaini.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment