Kigola akifurahi kabla kibao hakijageuka |
Nasifiwe Ponziano Miwoo mbele ya Waziri Nyalandu alipokuwa akihoji uadilifu wa mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola |
SAKATA
la vibali vya uvunaji miti katika msitu wa Taifa wa Sao Hill Mufindi
mkoani Iringa limemuweka pabaya mbunge wa jimbo la Mufindi kusini
Mendrad Kigola baada ya wapiga kura wake kumgeuka mbele ya waziri
maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa mbunge huyo ni mchochezi
katika sakata hilo.
Katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Igowole juzi Kigola
alimkaribisha waziri huyo huku akikosoa mgao wa vibali vya kuvuna miti
katika msitu wa Taifa wa saohill ambao sehemu yake upo katika jimbo
hilo, ulivyofanywa kwa vikundi vya wajasiriamali wa wilaya ya Mufindi.
Huku
akipigiwa makofi ya mara kwa mara yaliyomfanya ashindwe kusimama sehemu
moja wakati akiongea, Kigola alisema: “sina pingamizi dhidi ya watu na
vijiji vilivyopata mgao wa mwaka huu.”
“Shida
yangu ni mgao uliotolewa kwa vikundi vya wilaya ya Mufindi yenye
majimbo mawili. Wakati jimbo langu la Mufindi Kusini vimepata vikundi 12
kati ya 48, vingine vyote vilivyobaki vimetoka upande mwingine.
Mheshimiwa waziri, nakuomba ulione hilo,” alisema.
Kauli
ya Kigola ilitafsiriwa na baadhi ya watu waliokuwepo katika mkutano huo
kwamba ilikuwa ikimpiga vijembe mbunge wa jimbo jirani la Mufindi
Kaskazini, Mahamudu Mgimwa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii.
Taarifa
zisizo rasmi kutoka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya
Mufindi zinadai kwamba Mgimwa na Kigola hawapikiki chungu kimoja ikiwa
ni matokeo ya kinachoelezwa na walio jirani na wabunge hao kwamba mmoja
wao ana wivu wa kisiasa dhidi ya mwenzake.
Taarifa
hizo zisizo rasmi ambazo hata hivyo hazijawahi kutolewa ufafanuzi na
Kigola mwenyewe zinadai kwamba amekuwa akimuonea wivu Mgimwa baada ya
kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri.
Wivu
huo ndio umepelekea kuchochea chokochoko ya kuhoji uwiano wa mgao wa
vibali vikiwemo vibali 48 vilivyotolewa kwa vikundi 48 vya wilaya ya
Mufindi.
Hoja
ya Kigola dhidi ya mgao wa vibali hivyo ilionekana ina mashiko kwa muda
wote wa mkutano huo mpaka pale Waziri Nyalandu alipotoa ruksa kwa
wananchi wa kijiji hicho cha Igowole kuuliza maswali.
Alikuwa
Nasifiwe Ponziano Miwoo aliyechafua hali ya hewamara baada ya kupata
nafasi ya kuuliza swali alilotoa kwa mtindo aliodai wa kujenga hoja ili
wananchi wamuelewe.
Akinukuu vifungu kadhaa vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano huku akioanisha na uadilifu wa mbunge huyo Miwoo alisema:
“Kuna
haja ya kuoanisha hoja za mbunge huyu Kigola na uadilifu wake; na kuna
haja ya kujua mali zinazomilikiwa na mbunge huyu ili tuone kama
kunasababu kwa familia yake kupata kibali cha kuvuna miti wakati baadhi
ya vijiji na vya wilaya ya Mufindi na wajasiriamali wake wakikosa,”
alisema.
Alisema
katika orodha ya wanufaika na vibali vya mwaka huu, jina namba 388 ni
la mtoto wa Kigola anayesoma katika moja ya shule bora zilizoko wilayani
Mufindi.
Alisema
zipo dalili kwamba Kigola alitumia jina la mwanae huyo kupata kibali
hicho jambo linalojenga mashaka dhidi ya uadilifu wake.
“Mheshimiwa
Waziri tuna mashaka na huyu mtu na kama kila mwaka anajaza fomu
inayoonesha mali anazomilikia. Kwanini jina la mwanae litumike,” Miwoo
alisema huku waliokuwa wakimshangilia Kigola wakigeuza kibao na
kumshangilia yeye.
No comments:
Post a Comment