Tuesday, December 23, 2014

BALOZI IDDI AKAGUA JENGO LA SKULI YA SEKONDARI YA DONGE

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Donge kulia yeke Mh. Sadifa Juma Khamis, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa kushoto ya Balozi Seif  wakilikagua jengo la skuli ya sekondari la Donge ambalo limeanza kutua huduma. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge Maalim Khamis Mohamed.
 Jengo la Ghorofa mbili la Skuli ya Sekondari ya Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja ambalo tayari limeanza kuhudumia wanafunzi wa Sekondari baada ya kukamilika kwa hatua ya uezekaji.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge wakifuatilia hotuba ya kuzinduliwa  kwa Jumuiya hiyo kulikofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani. Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
*********************************************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha kwamba njia pekee wanayoitumia katika kuwarithisha hatma njema watoto wao ni kuwajengea msingi madhubuti wa kupata elimu.
Alisema suala la kusomeshwa kwa watoto halina mjadala kwani ni jambo la lazima bila ya kuzingatia au kuleta ubaguzi wa kijinsia kwa watoto wao wote.
Balozi Seif alisema hayo wakati akiuzindua uongozi mpya wa  Jumuiya ya Maendeleo Donge  hafla iliyofanyika katika viunga vya Skuli ya Sekondari ya Donge  iliyopo Wilaya ya Kaskazini “ B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema watoto wa kikazi kipya wanapaswa kufanana na wakati uliopo sasa na hili litafanikiwa ipasavyo endapo watoto hao watajikita zaidi katika masomo yao kwenye fani ya sayansi.
Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi na hasa Vijana kuelewa kwamba ajira za siku hizi katika Taasisi za Umma na zile Binafsi zinazingatia zaidi elimu ya vyuo vikuu yenye mnasaba zaidi na fani ya sayansi.
Alisema fani ya sayansi inayoonekana kupigwa chenga na vijana walio wengi maskulini bado ina upungufu katika Taasisi za Umma.
“ Watoto wetu lazima  wafanane na wakati huu. Na hili litawezekana na kufikiwa malengo yake kama juhudi za wazazi zitajikita katika kuwapatia taaluma inayofaa watoto wao “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Jumuiya hiyo ya Maendeleo pamoja na Wananchi wa Donge kwa jitihada zao za kuwajengea mazingira bora ya kielimu watoto wao.
Alisema ari hii ya wananchi wa Donge  ya kujenga Skuli inayofanana na hali ya sasa inatokana na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi wanaohitaji kupata fursa ya elimu.
Balozi Seif lifahamisha kwamba kitendo hicho kinathibitisha wazi kwamba Donge bado inaendelea kuongoza  kwa ubora wa elimu ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja tokea mwanzoni mwa miaka ya 60.
Katika kuunga mkono juhudi za Uongozi wa Jumuiya hiyo na wananchi wa Donge Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kutoa mchango wa  Saruji mifuko 200 pamoja na fedha za mafundi ili kupigwa plasta madarasa ya Skuli ya Sekondari ya Donge ambayo tayari wanafunzi wameanza kuyatumia.
Balozi Seif pia akawaahidi wananchi hao kuchukuwa jitihada za kuzungumza na washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi watakaoonyesha niya ya kutaka kusaidia ukamilishaji wa Skuli hiyo kubwa.
Akizungumzia muda mfupi ujao Balozi Seif aliwaeleza wananchi hao wa Donge kwamba Zanzibar inatarajia kusherehekea maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyokomboa wananchi wanyonge mwaka 1964.
Balozi alisema Wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wana kila sababu na haki ya kusherehekea maadhimisho hayo sambamba na kuendelea kuyalinda kwa nguvu  na gharama zao zote.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge Maalim Khamis Mohamed alisema Jumuiya hiyo imeanzishwa kwa lengo la kushirikiana na Serikali Kuu katika kuwaondoshea kero zinazowakabili Wananchi.
Maalim Khamis alisema licha ya Uongozi na wananchi hao kuanzisha mradi wa ujenzi wa Skuli lakini pia wamejikita kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi na hasa wakulima za upatikanaji wa huduma za kilimo pamoja na soko kwa mazao wanayozalisha.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge alisisitiza pia kwamba uongozi huo utaendelea kusimamia vyema rasilimali zilizomo ndani ya Jimbo la Donge na kuhakikisha kwamba zinawanufaisha kwanza wahusika hao.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Jumuiya na wananchi hao wa Donge Mlezi wa Jumuiya Hiyo Mzee Ali Ameir Moh’d aliwaasa viongozi wa Jumuiya hiyo kuwa makini katika utekelezaji wa jukumu walilokabidhiwa na wananchi wao.
Mzee Ali Ameir lisema ipo mifano mingi iliyoshuhudiwa katika maeneo mbali mbali nchini ya kuanzishwa kwa Jumuiya na kamati za Maendeleo lakini kinachoviza  utekelezaji wa Jumuiya na Kamati hizo ni ulafi wa madaraka  pamoja na itikadi za kisiasa kwa baadhi ya watu.
 Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata fursa ya kukagua Jengo la Skuli ya Sekondari ya Donge lenye Ghorofa mbili ambapo hivi sasa wanafunzi wameanza kulitumia katika sehemu ya chini baada ya kukamilika uezekaji.
Akimkaguza Balozi Seif kuliangalia jengo hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Jumuiya ya Mandeleo Donge Maalim Khamis alisema ujenzi wa jengo hilo ulioanza mwaka 1997 kwa michango na nguvu za wananchi wenyewe  umepangwa kufanyika kwa awamu tatu.
Mwenyekiti huyo kwa niaba ya Wananchi wa Donge alimpongeza na kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kupitia Balozi Seif kwa utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa katika kusaidia ujenzi wa skuli hiyo ya Sekondari Donge wakati alipoitembele

No comments:

Post a Comment