WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaambia watendaji na wadau wa mradi Mabasi
Yaendayo Haraka wa jijini Dar es Salaam (BRT) kuwa hawana muda wa kulala
wa kupumzika na akawataka wakamilisha haraka vipengele vichache
vilivyobakia ili mradi huo uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo.
Ametoa
agizo hilo jana usiku (Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na
wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao
alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.
“Watu wa
DART, UDA-RT hakuna muda wa kulala tena. Nanyi wa eGA, MAXCOM, POLISI NA
SUMATRA inabidi mfanye kazi kama timu moja na wenzenu ili maeneo
yaliyobakia yaweze kukamilika katika muda mfupi na kikubwa ni
kuhakikisha mnatoa elimu ya kutosha,” alisisitiza.
Akielezea
utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Ronald Rwakatare amesema miundombinu
ya mradi huo imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi
karibuni kwani hivi sasa wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji
nauli na uendeshaji wa mabasi hayo. Pia aliwatka wananchi kutunza
miundombinu ya mradi huo na kuwa makini na matumizi ya barabara wakati
mradi huo ukiwa kwenye majaribio na hatimaye kuanza kazi rasmi.
Alisema
watakuwa na karakana itakayotumika kwa ajili ya hayo mabasi ambayo
itakuwepo eneo la Jangwani na kwamba ofisi za mradi pia zitakuwa eneo
hilo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw.
Robert Kisena amesema mpango wa kuanza kwa mradi huo umekamilila na
tayari mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja na bima. UDA-RT ni kampuni ya
muunganiko wa UDA na wamiliki wa daladala ya kutoa huduma ya usafiri
katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka.
Bw.
Kisena amesema kesho wataanza majaribio ya mradi huo kwa kutumia mabasi
10 na watakuwa wanaongeza mabasi 10 kila siku hadi yafikie 50 hivyo
amewataka wananchi kuondoa shaka juu ya mradi huo. Naye, Mkurugenzi Mkuu
wa Maxcom Africa, Bw. Juma Rajab amesema mabasi hayo yatakuwa yanatumia
kadi za kielektroniki zitakazokuwa zinalipiwa kwa kutumia mitandao
mbalimbali ya simu za mkononi.
Bw. Rajab
amesema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba fedha za mteja zitakuwa salama na
hata kama atakapopoteza kadi yake. “Mtu akinunua kadi yake anapaswa
atunze namba ya usajili iliyoko kwenye kadi hiyo kwani itatumika
kurudishia fedha zake kupitia namba yake ya simu ya mkononi,” alisema.
Amesema
Maxcom Africa ndio wakusanyaji wa nauli kwa kushirikiana na UDA-RT
ambapo watatumia mawakala wa MaxMalipo hivyo kila mwananchi atapata
fursa ya kununua kadi yake kwa urahisi. Alisema taarifa za kila mtumiaji
zitaunganishwa na simu yake ya mkononi ambapo mhusika ataweza kujua kwa
urahisi salio la fedha lililomo kwenye kadi yake.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAMOSI, APRILI 16, 2016.
No comments:
Post a Comment